Morogoro Yapokea bil. 5/- za Miamala ya Simu




MKUU wa Mkoa wa Morogoro, Fatma Mwassa, amesema kuwa mkoa huo umepokea Sh. bilioni 5.5 za mgawo wa miamala ya simu kwa kipindi cha 2021/2022 kwa ajili ya ujenzi wa vituo 11 vya afya.

MKUU wa Mkoa wa Morogoro, Fatma Mwassa.
Akizungumza wakati wa kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC), kilichofanyika mjini hapa, alisema kutokana na mgao huo sasa ujenzi unaendelea lengo ni kuhakikisha wananchi wanapata huduma muhimu.

Akifafanua zaidi, Katibu Tawala Msaidizi Idara ya Mipango na Uratibu mkoa huo, Anza -Amen Ndossa alisema wanasimamia kwa karibu ujenzi wa majengo husika.

Ndossa alifafanua kuwa hali ya utekelezaji kwa vituo hivyo vilivyopata fedha awamu ya kwanza ilifikia asilimia 95 na kwa vituo vya awamu ya pili umefikia asilimia 25 na ujenzi wake bado unaendelea na kwamba kila kituo kimepatiwa Sh. milioni 500.

Aidha, alisema kata zilizochaguliwa baadhi zinaidadi kubwa ya wakazi na nyingine zipo pembezoni kutoka makao makuu ya halmashauri husika na kutokuwa na vituo vya afya kwa ajili ya huduma za wananchi.


Ndossa alizitaja halmashauri zilizopatiwa fedha na idadi ya vituo kwenye mabano na kata zake ni Malinyi (1) Ulanga (1), Mlimba (1) na Mji Ifakara (1).

Nyingine ni Kilosa (2), Gairo (1) Mvomero (1), Manisapaa ya Morogoro (1) na Morogoro (2).

Katika hatua nyingine, alisema halmashauri za mkoa huo zilitekeleza agizo Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kutenga Sh bilioni 2.6 kutokana na fedha za mapato ya ndani kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya afya.


Alisema kati ya fedha hizo, halmashauri ya wilaya ya Malinyi ilitenga kiasi cha Sh. milioni 574 za ukamilishaji hospitali ya wilaya na kituo cha afya Ngoheranga na Halmashauri ya Ulanga ilitenga Sh. milioni 100 za ujenzi wa zahanati mbili.

Ndossa alizitaja nyingine na kiasi kwenye mabano kuwa ni Mlimba (milioni 500), Mji Ifakara (milioni 410), Mvomero (milioni 200), Morogoro (milioni 310) na Manispaa ya Morogoro (milioni 570) huku Kilosa haikutenga na Gairo haikupangiwa mradi.

Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Mikumi, Dennis Londo akichangia katika sekta ya afya aliushauri mkoa na wilaya ya Kilosa kuweka mipango ya kujenga kituo cha afya kata ya Ruaha ,tarafa ya Mikumi.

Mbunge huyo alisema kata hiyo ina idadi kubwa ya watu na shughuli nyingi za uwekezaji kikiwemo kiwanda cha Sukari Kilombero ambacho kinapokea watu wengi ambao wanaishi kwenye kata hiyo ambayo haina kituo cha afya.


Akizungumza katika kikao hicho, Mkuu wa mkoa huo, Mwassa alimwagiza mganga mkuu wa mkoa kulifanyia kazi jambo hilo, ili katika kata hiyo kijengwe kituo cha afya cha kisasa cha kutoa huduma za afya kwa wananchi na wageni.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad