KUNA ukweli ambao mashabiki wa Simba wengi hawataki kuusikia kwa kuwa wameaminishwa msimu huu wana kikosi bora sana.
Lakini ukisimama karibu na uwanja ukachunguza vizuri ufanisi wa kikosi cha kwanza na halafu ukageuka nyuma kuangalia wanaopasha pale benchi kisha walioko jukwaani utagundua kuna sehemu kuna tatizo.
Simba inahitaji wachezaji mbadala wenye uwezo wa kuipa matokeo bora. Yaani kikitoka kitu kiingie kitu. Wako ambao wanaona makocha Juma Mgunda na Selemani Matola hawatoshi lakini ukileta kocha wa kigeni pia atahitaji usajili bora haswa wachezaji mbadala wa kikosi cha kwanza.
Mgunda na Matola wanatakiwa kupongezwa zaidi kwa kazi walioifanya mpaka sasa kitu kilichosalia sasa ni uamuzi wa Bodi ya Simba kuwasajilia watu mbadala waliobora kwa kuwa changamoto za kikosi zimeshakuwa hadharani. Simba pia inapaswa kuboresha benchi la ufundi kwa kutafuta kocha wa viungo atakayekuja kuchukua nafasi ya Sbai Karim ambaye alishaondoka, benchi lao halijakamilika kama walipokuwa na mafanikio makubwa.
Hata kitengo cha utabibu nacho kinatakiwa kuangaliwa kama kuna watu mwafaka kwani kunaendelea kuongezeka kwa wachezaji wenye majeraha hali ambayo inaiumiza timu hiyo huku nguvu kubwa ikiwa chini kupokea matibabu yasiyokwisha.
Ndiyo, Simba imetinga hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika ikiwa na kikosi hiki ambacho kiuhalisia kina changamoto za ubora na hapa ndipo unapokuja kuona Wekundu hao walikuwa na bahati katika safari yao.
UZOEFU KIMATAIFA
Simba kutinga makundi sio kitu chenye presha kwao kwa sababu kuna wachezaji wengi ambao wameishi katika mechi hizo kubwa na wala haikuwa kitu kigumu kwao hasa walipokutana na timu changa kama Nyassa Big Bullets ya Malawi na hata Primeiro de Agosto ya Angola.
Kwa ubora wa kikosi cha Simba ukiongeza na uzoefu wa viongozi wao hizi hazikuwa mechi ngumu kiasi cha kuwazuia kutinga makundi kwani walikuwa na kila silaha ya kuitumia.
Swali ambalo viongozi wa Simba watasema hapa hawawezi kuingia makundi wakiwa na kikosi kama hiki bila kuongeza wachezaji bora kama wawili au watatu.
WASHAMBULIAJI WANAHITAJIKA
Wakati wa dirisha la usajili Simba ilipiga hesabu rahisi kwa kuwasajili washambuliaji Habib Kyombo, Dejan Georgijevic, viungo, Victor Akpan, Nelson Okwa, haukuwa usajili ambao umeibeba ni sawa na kusema matarajio yao yalishindwa kufikiwa.
Hili halitokei Simba tu ni duniani kote lipo na huu sio wakati wa kulaumiana, mpira ni mchezo wa wazi warudi chini kwa utulivu na kufanya upembuzi wa kina kisha waingie sokoni kwa tahadhari na sio mihemko kwani wanapata watu waliobora zaidi kwa mahitaji ya timu.
WAKONGWE WATEMWE
Wapo wachezaji wanaoonekana umri kuwatupa mkono, hili nalo sio jipya, Simba waliangalie kwa kina kama wataona mchango mdogo kwa wachezaji ambao waliwapa mafanikio hata kama ni wazawa waachane nao kwa heshima kama walivyofanya kwa Meddie Kagere na hata Thadeo Lwanga.
Mpira ni mchezo wa umri na hatua ambazo Simba inaenda kucheza ni ngumu na inahitaji wachezaji wenye kasi na nguvu ya kupambana, kama itaamua kutoachana na hao wachezaji wakongwe, basi iamue kutowafanya kuwa tegemezi.
TIMU HAINA UWIANO
Usajili uliopita Simba ilisajili kwa papara na kukosa uwiano wa ushindani wa mchezaji kwa mfano viungo wakabaji ndani ya kikosi hicho anza na Akpan, Jonas Mkude, Nassoro Kapama, Mzamiru Yassin na Sadio Kanoute. Kwenye lundo la viungo wakabaji watano utaona hesabu za usajili hazikufanyika kitataalam hakuna hata mmoja ambaye angeweza kucheza kama kiungo mshambuliaji wa juu na akafanya kitu kikubwa.
Ukija katika viungo wa juu wachezeshaji walikuwa na Okwa na Chama ambapo Okwa ameshindwa kuonyesha ubora wake na kubaki na Chama kibaya zaidi naye amefungiwa mechi tatu ina maana hakuna mtu tena.
Uhalisia wa hilo unaupata katika kikosi cha sasa ambapo kati ya wachezaji 27 waliopo kikosini, 17 kiasili ni mabeki na 10 ndio wa nafasi za ushambuliaji wa kati na viungo washambuliaji.
PHIRI, OKRAH
Mbele ndio kuna mashaka zaidi tegemezi limebaki kwa Phiri na Augustine Okrah kidogo, ndio wamekuwa wakifunika udhaifu wa wengine. Katiuka mechi tano zilizopita Phiri amefunga mabao matano, akishindwa kufunga dhidi ya Yanga, Azam, Singida Big Stars na Ihefu huku akifunga dhidi ya Mtibwa.
Okrah naye katika mechi hizo amefunga bao dhidi ya Yanga na nyingine akikosekana kabisa japo hadi sasa ana jumla ya mabao matatu. Kibu Denis na Habib Kyombo ndio kama vile unaweza kufurahia unapowaona wanapasha lakini wakishaingia ni viugumu kutabirika kama watakupa unachohitaji.
Ukiondoa Okrah na Phiri ambao wanaonekana kuisaidia timu, Nasoro Kapama, Nelson Okwa, Mohamed Ouattara, Kyombo na Victor Akpani wameshindwa kuisaidia timu. Simba iachane na usajili wa ‘kidalali’ wa wachezaji kuimbwa sana kwenye mitandao kisha kuwashawishi mashabiki hizi ni mbinu ambazo zimepitwa na wakati, Simba ina bodi ya watu wanaojua mpira waache kupigana shoti wakatulie na kufanya maamuzi yenye afya katika dirisha dogo.
WAFUNGAJI
Simba inatakiwa kurudi sokoni kutafuta wafungaji wenye ubora kazi ambayo haihitaji kukurupuka watangulize utulivu ni bora wakate lundo la wachezaji wa kawaida kisha wakatumie bajeti inayokidhi soko kuwapata watu bora wa ufungaji kuirudishia timu hadhi yake uwanjani. Ili kutinga nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika inahitaji wachezaji wa kutembeza boli na kutupia.
NUSU FAINALI
Kufika hatua hii Simba ya Ligi ya Mabingwa Afrika inahitaji kuwa na malengo kama hayo lakini kwa ubora wa kikosi chao utagundua hakina uhalisia wa kufika huko kama tu kilishindwa hata kupata pointi mbili katika mechi za kikubwa dhidi ya Azam, Yanga na Singida.
Simba inakwenda kucheza mechi ngumu za makundi ambazo wanatakiwa kukumbuka mara ya mwisho waliposhiriki hatua kama hiyo walikuwa na kikosi chenye ubora upi, wakipata majibu waanze kuangalia akaunti yao ina afya gani kuweza kuingia sokoni haraka kwani kupanga ni kuchagua.