Dar es Salaam. David Rubaga, mtoto mkubwa wa marehemu rubani Buruhani Rubaga ameeleza walichozungumza na baba yake kabla ya safari.
Rubaga alikuwa rubani wa ndege ya Precision Air iliyoanguka Jumapili Novemba 6, 2022 asubuhi katika Ziwa Victoria karibu na uwanja wa ndege wa Bukoba na kusababisha vifo vya watu 19 na 24 wakinusurika.
Akizungumza na Mwananchi jana Jumatano Novemba 9, 2022, David amesema siku moja kabla ya ajali hiyo kutokea walizungumza mambo mengi na baba yake ikiwamo ya familia na kazi.
Amesema baba yake alimuasa mambo mengi ya kumfariji katika maisha huku akimtaka kuwa na uvumilivu.
“Kwa ukweli msiba tumeupokea kwa masikitiko makubwa, siku moja kabla ya ajali tulizungumza sana kwa simu dakika 43, masuala ya familia na kazi.
“Kiukweli aliniasa mambo mengi ikiwa ni kuwa na subira, maisha yanenda taratibu na lazima niwaangalie watoto na niwajengee msingi watoto” amesema David.
David ambaye ni mtoto mkubwa kati ya watoto saba wa marehemu Rubaga amesema kuwa mazungumzo yao yalikuwa na tija na yanamuumiza akiyakumbuka.
“Kiukweli mazungumzo yalikuwa na tija sana ambayo yataniongoza na pia yananiumiza” amesema
View this post on Instagram
A post shared by Mwananchi (@mwananchi_official)
Jana wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu ajali hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafri wa Anga Tanzania (TCAA), Hamza Johari alimtaja Rubaga kuwa miongoni mwa marubani bora nchini.
Johari alisema hadi ajali hiyo inatokea kapteni Rubaga alikuwa amekusanya saa 23, 515 za kuruka na alikuwa mwanzilishi wa kwenda na ndege kubwa katika uwanja wa Bukoba.
“Hadi ajali inatokea kapteni Rubaga (Buruani) alikusanya saa 23, 515 za kuruka alikuwa ni mmoja wa marubani bora nchini, lakini pia alikuwa mwanzilishi wa kwenda na ndege kubwa katika uwanja wa Bukoba na mwalimu wa marubani wenzake wa namna ya kutua na kuruka katika uwanja ule” alisema Johari.