Mufti: Punguzeni dhambi mvua zinyeshe



Dar es Salaam. Mufti wa Tanzania, Sheikh Abubakar Zubeir amewaasa Watanzania kupunguza na kuacha kabisa kutenda dhambi na badala yake wamrudie Mwenyezi Mungu ili kuwaepusha na adha ya ukame ulioikumba nchi.

Amesema kukosekana kwa mvua, uwepo wa ukame na kukauka kwa maji ardhini ni ishara kwamba watu wanatenda maasi.

Hata hivyo mabadiliko ya tabianchi yanatajwa kuwa ni sababu ya ongezeko la joto, mvua zisizotabirika pamoja na ukame.

Mufti ameyasema hayo leo Jumamosi Novemba 5, 2022 alipokuwa akiongoza dua maalum ya maadhimisho ya miaka 26 tangu kuanzishwa kwa Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (MOI).


“Tunapoomba mvua tuendelee kuacha maasi na mambo mengine yasiyofaa, watu waache dhuluma, mambo mabaya yanayosababisha sisi Mwenyezi Mungu atunyime mvua,” amesema Mufti Zuberi.

Amesema tayari viongozi wa dini wameanza kuomba dua kwa ajili ya kuiombea mvua.

“Mwenyezi Mungu atuletee mvua yenye kheri isiyo na maafa kwetu Tanzania na nchi zingine zilizopakana na sisi. Tunajipanga kuomba dua kwa Watanzania kwa ujumla na wenzetu wengine watafanya dua siku ya Jumatatu.


“Wananchi wote kila mmoja kwa nafasi yake aombe dua ili tupate mvua isiyo na maafa tushirikiane katika kumuomba Mwenyezi Mungu hii itakaribisha baraka na itatuondoshea huu wasiwasi viongozi wote wa dini, mashekhe wote tushirikiane,” amesema Mufti Zubeir.

Paroko wa Kanisa Kuu la Mtakatifu Joseph, Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Padri Denis Bwigira amesema Mungu amejalia vitu vingi vya asili binadamu aweze kuvitumia kwa akili lakini wakati huu kwa pamoja viongozi wa dini wapo katika kuomba kwa sala makanisa yote.

“Naamini kutakua na maombi ya kitaifa. Tanzania tuna utajiri mkubwa wa maji ardhini na kwenye maziwa tumuombe Mungu atuzidishie uwezo wa kiteknolojia tuvute maji yaliyopo ardhiri tunaamini Mwenyezi Mungu hawezi kutuacha tuangamie kwa kiu,” amesema na kuongeza;

“Tunaamini tutapata maji ya kutosha na hii itukumbushe tunapo mtumainia Mwenyezi Mungu kuna njia za kujiwekea imani ya kuwa makini kwa majanga mbalimbali.”


Sala hiyo imehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa taasisi za tiba pamoja na viongozi wa kidini ambao kwa pamoja wameitaka taasisi hiyo kuendelea kutoa huduma kwa upendo, na kufuata maadili ya utumishi wa umma.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad