Zifahamu ajali 5 mbaya zaidi kuwahi kutokea Tanzania




Ajali ya ndege ya Precision Air iliyotokea Bukoba, nchini Tanzania na kuua watu 19, ni moja ya ajali nyingi zinazotokea katika maeneo mbalimbali.

Mkaguzi Mkuu wa Ajali za Ndege nchini humo, kutoka Wizara ya Mawasiliano na Uchukuzi, David Nyamwihura aliwahi kunukuliwa na gazeti la Mwananchi nchini Tanzania kwamba, ripoti ya ajali za ndege hapa nchini humo inabainisha kuwa tangu mwaka 1920 hadi 2013 zimewahi kutokea ajali 52 zilizosababisha vifo vya watu 196. Na idadi kubwa ya ajali hizo hutokea maeneo ya milimani.

Lakini ajali ya sasa imetokea katika ziwa Victoria, mita chache kutoka uwanja wa ndege wa Bukoba, wakati ndege ya Precision Air PW 494 ikijiandaa kutua ikitokea Dar es Salaam kupitia Mwanza.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, amesema serikali itafanya uchunguzi kubaini chanzo hasa cha ajali hiyo, iliyoibua simanzi kwa watanzania.



Maelezo ya picha, Ajali ya ndege ya Precision Air Bukoba ilua watu 19
Pamoja na kwamba ni ajali ya ndege iliyoanguka ziwani, imekumbusha machungu ya ajali nyingi kubwa zilizowahi katika maeneo mbalimbali na kupoteza idadi kubwa ya watu.

Hakuna asiyesahau vifo vya watu zaidi ya 100 walioungua na moto wa mlipuko wa gari la mafuta mkoani Morogoro. Lakini vifo vya wanafunzi zaidi ya 30 wa shule ya Lucky Vincent, Arusha kwenye ajali ya basi dogo iliyotumbukia katika mto Marera ulioko katika mlima Rhotia, Karatu nayo ilileta simanzi kubwa.

Ajali nyingi zimetokea barabarani, angani na majini, lakini hizi tano zitaendelea kukumbukwa zaidi nchini Tanzania.


5: MV Skagit - 2012
Ajali hii ilitokea miezi 10 tu baada ya kutokea kwa ajali ya MV Spice Islander. Ilikuwa Julai 18, 2012 majira ya alasiri meli hii ya MV SKAGIT ilipozama katika eneo la Chumbe, Zanzibar. Meli hiyo iliyokuwa ikitokea Dar es Salaam kueleka Zanzibar ilikuwa imebeba watu 290. Kati yao watu wazima 250, watoto 31 na wafanyakazi wa meli 9.

Wananchi walikumbushwa machungu ya ajali ya MV Spice Islander kwa ajali ya meli ya Skagit iliyoua watu 81, wakiwemo Watanzania 75, Wakenya 3, Waholanzi 2 na Mrundi 1. Aidha, watu 212 walipotea na 154 walinusurika wakiwemo Waholanzi 5, Wajerumani 4, Wabelgiji 2, Wamarekani 2 na Waisraili 2. Kwa mujibu wa ripoti tumwe iliyoundwa kuchunguza ajali hiyo

Chanzo cha Meli hii iliyoundwa nchini Marekani mwaka 1989 na kampuni ya HALTER MARINE kuzama inaelezwa ilikuwa ni kutokana na hali mbaya ya hewa.

4: Ajali ya Treni -Msagali - 2002
Dodoma
Maelezo ya picha, Ajali ya treni iliyotkea Msagali Dodoma ni moja ya ajali kubwa za treni Tanzania
Kwenye upande wa ajali mbaya za treni kuwahi kutokea Tanzania hii ni miongoni mwao. Ajali ya treni ya abiria Namba A.12 ilitokea kilomita 388 kati ya stesheni za Igandu na Msagali Juni 24, 2002 saa 2.30 asubuhi.


‘Taifa limekumbwa na msiba mkubwa’ hii ilikuwa sehemu ya taarifa fupi kuhusu ajhali hiyo aliyowasilisha waziri wa uchukuzi wakati huo Profesa Mark Mwandosya, bungeni Dodoma.

Watu 281 walipoteza maisha, maiti 193 zilitambuliwa na kuchukuliwa huku maiti 88 zilizikwa na mamlaka za serikali kwenye mazishi ya halaiki katika makaburi ya Maili Mbili Kata ya Miyuji mjini Dodoma 27 Juni 2002 kutokana na kutotambuliwa.

Inaelezwa treni hi ilikosa nguvu ya kupandisha muinuko na breki kushindwa kufanya kazi kabla ya kuanza kurudi kwa kasi kinyumenyume na kwenda kuvaana na treni nyingine ya mizigo.

3: MV Nyerere - 2018

Maelezo ya picha, Kivuko cha MV Nyerere kilikuwa na uwezo wa kubeba watu 101 lakini siku ya ajali ilielezwa kujaza watu karibu mara mbili ya uwezo wake
Septemba 2018 jumla ya watu 224 walifariki na watu wengine 41 wakiokolewa wakiwa hai katika ajali ya kivuko cha MV Nyerere.


Ilikuwa moja ya ajali iliyoleta kumbukumbu ya ajali kubwa zaidi ya MV Bukoba. Iliyotokea katika ziwa hilo hilo.

Mhandisi wa kivuko hicho Alphonce Charahani alikuwa wa mwisho kuokolewa akiwa akiwa hai baada ya kukaa majini kwa saa 48.

Rais wa wakati huo hayati John Magufuli alipozungumza alieleza kuwa kivuko hicho cha MV Nyerere kilikuwa na uwezo wa kubeba abiria 101, lakini kwa takwimu za miili iliyopatikana na pamoja na manusura, ni wazi kwamba chombo hicho kilikuwa kimebeba abiria wengi kuliko uwezo wake.

2: MV Bukoba - 1996
Hii ni ajali ya kihistoria, pengine ni moja ya ajali iliyoua watu wengi zaidi kwa wakati mmoja kuwahi kutokea Tanzania katika miongo ya hivi karibuni. Ilitokea Mei 21, 1996, na hata Serikali iliwahi kukiri kwamba ajali hiyo itaendelea kuwa miongoni mwa kumbukumbu mbaya kutokana na kuangamiza maisha ya mamia ya Watanzania wengi kwa wakati mmoja.

Inakadiriwa kuwa zaidi ya watu 800 walifariki katika ajali hiyo iliyotokea kilomita chache kutoka bandari ya Mwanza.


Ingawa ni miaka 26 sasa tangu kuzama kwa meli ya MV Bukoba, Bukoba ilipokuwa inakaribia bandari ya Mwanza umbali wa kilometa 56, aliyekuwepo na asiyekuwepo historia yake imeendelea kukaa vichwnai mwa wengi.

Meli hiyo iliyoundwa mwaka 1979 ikiwa na uwezo wa kubeba mizigo tani 850 na abiria 430 iliyokuwa tegemeo kubwa la kutoa huduma ya kubeba mizigo na abiria ndani ya Ziwa Victoria kati ya Bandari za Bukoba na Mwanza. Siku ya ajali inaelezwa kupakia zaidi ya abiria 2,000.

1: MV Spice Islander - 2011
Spice
Pengine kumbukumbu ya muda mrefu ya ajali ya MV Bukoba inapunguza machungu ya ajali ya MV Spice Islanders. Kuzama kwa meli ya MV Spice Islander hapo Septemba 10, 2011 katika eneo la Nungwi, Kaskazini mwa kisiwa cha Unguja, kulileta huzuni kubwa hasa visiwani humo kutokana na idadi kubwa ya watu kufariki.

Kwa mujibu wa ripoti rasmi ya jopo lililoundwa kuchunguza ajali hiyo chini ya Jaji Abdulhakim Ameir aliyeongoza jopo la watu 10, watu 1370 walipoteza Maisha.

Uchunguzi unaeleza ilibeba abiria karibu mara nne Zaidi ya uwezo wake. Ilikuwa na abiria 2,470 wakati uwezo wake ilikuwa watu 620.

Tume iliyoundwa inasema meli hiyo ilibainika kuwa na hitilafu iliyojulikana miezi miwili kabla ya kuzama kwake kutokana na ukaguzi uliofanywa na taasisi ya usalama wa bahari Sumatra, lakini bado meli hiyo ilipewa leseni.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad