Nabi mguu ndani, mguu nje Yanga




HALI tete Yanga, baada ya matokeo ya suluhu waliyoyapata katika mchezo wa juzi dhidi ya Club Africain ya Tunisia, inamuweka katika wakati mgumu Kocha Mkuu wa timu hiyo, Nasreddin Nabi.

Yanga ilipata matokeo hayo katika mechi ya kwanza ya hatua ya mchujo wa Kombe la Shirikisho Afrika (CAFCC), iliyochezwa katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Matokeo hayo yamewaweka katika mazingira magumu wanapokwenda katika mchezo wa marudiano, mchezo utakaochezwa Novemba 9, katika Uwanja wa Hammedi Agrebi Olympic nchini Tunisia.

Kabla ya mchezo wa juzi, kulikuwa na taarifa kuwa kocha huyo amepewa dakika 180 dhidi ya Club Africans ili kunusuru kibarua chake hivyo amebakisha dakika 90 tu ambazo anatakiwa kuibakisha timu katika michuano hiyo.

Habari za uhakika kutoka ndani ya klabu ya Yanga, zinadai kuwa kocha huyo akishindwa kuipeleka Yanga katika hatua ya makundi, uongozi umepanga kuvunja mkataba wake.


“Makubaliano ya mwisho ilikuwa ni kuipeleka timu hatua ya makundi, hata yeye aliahidi hivyo,” zilieliza habari hizo.

Akizungumzia kuhusu kibarua chake Yanga, Nabi alisema anaamini bado anauwezo wa kuonesha uwezo katika mchezo ujao.

Alisema anaamini mpira unadunda, Club Africain walicheza mpira wa kujilinda zaidi hata wao watakwenda na mbinu mbadala kuhakikisha wanafanya vizuri.


“Tulipania kufanya vizuri katika mchezo wa nyumbani, wenzetu walijilinda sana na naamini hawawezi kucheza hivyo katika mchezo wa marudiano, tunakwenda kupambana kuhakikisha tunashinda ugenini,” alisema Nabi.

Alisema walishindwa kupata mabao kutokana na wapinzani wao kucheza zaidi kwa kujilinda, kwa ubora wa kikosi chao wana uwezo wa kupata matokeo mazuri katika mechi ya marudiano.

“Huwezi kupata mabao dhidi ya timu inayocheza na wachezaji tisa nyuma (kujilinda), tunaamini kwao hawatacheza namna hii na watafunguka kwa ajili ya kusaka ushindi.

“Tunaamini ubora wa wachezaji wetu na jinsi tulivyomuona mpinzani wetu na kitu cha kufanya kwenye mechi ya marudiano kuwa makini safu ya ulinzi na ushambuliaji kutumia vema nafasi ili tufuzu na kusonga mbele katika mashindano haya," alisema Nabi.


Mtendaji Mkuu wa Yanga, Adre Mtine, alisema wanamtambua Nabi bado ni kocha mkuu wa timu hiyo na ataendelea kukinoa kikosi chao.

“Niwaombe mashabiki na wanachama wetu kuwa na utaratibu wa kufuatilia taarifa za klabu yetu kutoka kwenye vyanzo vyetu vya habari,” alisema.

Wakati huo huo, Makamu Rais wa Club Africain ya Tunisia, Mehdi Gharbi amekiri kukutana na timu nzuri ya Yanga, hasa kwenye upande wa ushambuliaji na viungo, lakini akasema itakuwa ni ngumu kwao kupata ushindi nchini kwao.

Akizungumza juzi baada ya mechi hiyo alisema wanashukuru kwa suluhu waliyoipata kwani ndiyo ilikuwa ni mpango mkakati wao baada ya kuwasoma vizuri wapinzani wao.


"Ilikuwa ni mechi ngumu, tukiri kuwa tumekutana na timu nzuri ya Yanga, kwa hii suluhu tuliyoipata tunashukuru Mungu kila kitu kitafanyika nyumbani kwenye mchezo wa marudiano. Yanga wana mastraika na viungo wazuri sana, na tuliwasoma vizuri, hivyo tulivyokuja huku mpango mkakati wetu ulikuwa ni kuwazuia ili tutoke suluhu na nimefanikiwa," alisema Gharbi.

Kutokana na matokeo hayo alisema wana matumaini makubwa ya kushinda kwenye mechi ya marudiano.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad