Dodoma. Mkutano Mkuu wa uchaguzi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Dodoma umemchagu la Mbunge wa Kongwa, Job Ndugai kuwa mwenyekiti wa muda wa mkutano huo.
Uchaguzi wa Ndugai umekuja kufuatia klanuni ya uchaguzi kwamba mwenyekiti kama anagombea basi atalazimika kupisha nafasi hiyo na mkutano utamchagua mtu mwingine kukalia kiti hicho kuendesha mkutano.
Leo Jumatatu Novemba 21, 2022 mara baada ya kujiuzulu kwa aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Dodoma, Godwin Mkanwa, msimazi alitaka wajumbe wachague mwenyekiti wa muda.
Hata hivyo, ukumbi mzima kelele zilisikika wengi wakimtaja Ndugai kuwa aende mbele na hata walipotaka wajumbe kutulia ili wataje majina, watu walipiga kelele na wengine wakasimama wakitaka Ndugai asiwe na mpinzani.
Hali ilipokuwa hivyo huku wakiimba mlete Ndugai, mlete Ndugai ndipo wanachama wengi walisimama na Naibu Meya wa Jiji la Dodoma Jamal Ngalya walikwenda kumnyanyua Spika huyo Mstaafu na kumpeleka mbele.
Akizungumza mara baada ya kukalia kiti, Ndugai amesema atawatendea haki wagombea wote na kuwapa haki yao mbele ya wajumbe
Hata hivyo, Ndugai kama kawaida yake aliwatania wajumbe kuwa atakwenda kwa spidi kama ilivyo timu ya Simba jambo lililozua kicheko ukumbi mzima wengine wakisema hapanaaaa.