Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) kipo mbioni kununua ndege mbili kwa ajili ya kuwafundishia marubani.
Hayo yameelezwa Novemba 3,2022 na Mkuu wa Chuo hicho, Prof. Zacharia Mganilwa wakati akieleza taarifa ya chuo hicho kwa mwaka wa fedha 2022-2023 pamoja na vipaumbele vyake.
Prof amesema katika Mwaka wa Fedha, 2022/23, Chuo kinanunua tena ndege yenye injini mbili kwa ajili ya mwanafunzi kukamilisha mafunzo Yao.
“Kwa sababu mafunzo ya Urubani yanamtaka mwanafunzi ajifunze ndege yenye injini moja na injini mbili,”amesema Prof. huyo.
Amesema kumfundisha Rubani mmoja nje ya nchi ni Sh milioni 200.
“Hivyo Serikali inapofanya uwekezaji huu inalifanya Shirika la Ndege Nchini kuleta matumaini ya nchi katika kukuza utalii na uchumi kwa sababu Wataalam wa usafiri wa anga watafundishwa hapa hapa nchini,”amesema.
Amesema Serikali imekopa takriban Shilingi bilioni 49 kutoka Benki ya Dunia kwa ajili ya Kituo ncha Umahiri cha Mafunzo ya Taaluma za Usafiri wa Anga na Operesheni za Usafirishaji.
Amesema Chuo hicho kina majukumu ya kutayarisha Wataalam wa Sekta ya Usafiri wa mAnga.
“Fedha hii imegawanywa katika upande wa ujenzi wa miundombinu kwa ajili ya kufundishia n Wataalam ambapo jumla ya majengo matano yatajengwa Dar es Salaam kwa gharama ya Shilingi bilioni 21.
“Na baadae tutajenga majengo mkoani Kilimanjaro kwa sababu lazima Marubani wafundishiwe ndani ya Viwanja vya Ndege,”amesema
Amesema fedha nyingine itatumika kununua vifaa vya mafunzo, kwa kuwa Kituo kitafundisha Marubani, Wahandisi wa Ndege, Wahudumu Ndani ya Ndege na Waajiriwa wa Viwanja vya Ndege.
Mkuu huyo wa chuo amesema Tanzania ina zaidi ya ndege 400 zilizosajiliwa na Mamlaka ya Usafiri wa Anga ambapo asilimia 60 ya Marubani ni wageni.
“Hivyo ndege hizi zitakapofika vijana wa kitanzania wenye sifa za kusomea Urubani watafundishwa na kupata ajira ndani ya nchi,”amesema
Amesema Serikali inaendelea kukuza Uchumi wa Buluu, hivyo kupitia uwekezaji wa mradi wa Benki ya Dunia wameweza kusomesha Wataalam.
Amesema kwa mara ya kwanza tangu Uhuru, chuo kinafundisha pia Diploma ya Uchomeleaji na Uungaji wa Bomba la Mafuta.
“Hii itasaidia tusipeleke tu madereva na kina mama lishe bali tupeleke pia Wataalam watakaokuwa wanachoma bomba la mafuta”amesema.
“Tuna Kituo kingine cha Umahiri cha Kikanda katika usalama Barabarani ambacho kinafadhiliwa na Benki ya Maendeleo ya Afrika kwa Dola za Marekani Milioni 2.1 kwa mradi wote,”amesema.
Amesema kwa mwaka wa masomo wa 2022/23, tunatarajia kufikisha wanafunzi 14,000.
Kwa upande wake,Msemaji Mkuu wa Serikali,Gerson Msigwa alisema Serikali iliamua iwe na Chuo cha Usafirishaji kwa sababu kuendesha vyombo vya moto ni taaluma na ujuzi.
Amesema kuna miongozo inayotakiwa kuzingatiwa, kinyume cha hapo ni hatari.
Amesema NIT watawezesha vijana kunufaika na miradi mikubwa inayoendelea nchini mathalan ndege tano zinazotarajiwa kuja nchini, ambapo kwa mwaka 2023, ndege nne zitaingia nchini.