"MAISHA ya hapa Zanzibar ni mazuri sana kuliko ambayo ningeendelea kuishi nyumbani kwetu Kiev (Ukraine)," Vladyslava Yanchenko (23), raia wa Ukraine anasimulia utofauti wa maisha ya Zanzibar na nchi aliyotoka.
Vladyslava ambaye sasa anaishi Kijiji cha Kizimkazi Dimbani, Mkoa wa Kusini Unguja baada ya kukwama kurejea kwao kutokana na vita, anaendeleza simulizi ya ushuhuda wake, akitamka:
"Kwa kuishi hapa Zanzibar nimejua kufua, kulima na kujipikia. Kule kwetu Kiev zinasikika sauti za mabomu na risasi, hakuna amani, muda wote ni wasiwasi."
Binti huyo ni miongoni mwa watalii 1,200 ambao wakati vita inatokea, walikuwa visiwani Zanzibar kwa shughuli za utalii. Baadhi waliondoka kwenda maeneo mbalimbali duniani na wengine walibaki na kusaidiwa na serikali kupata visa na sehemu za kuishi.
Vladyslava alipata unafuu kuwa siku za nyuma katika safari zake za utalii, alipapenda Zanzibar na kununua ardhi kwa ajili ya uwekezaji, hivyo kulipotokea vita, alijenga nyumba ya kawaida kwenye eneo lake na ndiko anakoishi kwa sasa.
Anasema katika maisha yake hakuwahi kufikiri kuna siku angeishi kijijini kwenye maisha ya kawaida kabisa ya Kiafrika na akamudu kujipikia, kufua na kulima mazao yanayomsaidia, lakini imetokea na sasa amekuwa swahiba wa wenyeji wa Zanzibar.
Vladyslava, katika mazungumzo mahususi na Nipashe visiwani Zanzibar, anasema kwa sasa ameshakuwa mwenyeji na anaendesha biashara zake mtandaoni na kujipatia kipato cha kuendesha maisha yake.
Anasema anafurahi maisha yake mapya kwenye eneo lisilo na msongamano na shughuli nyingi kama ilivyo Kiev.
"Nimepita kipindi kigumu sana cha maisha, msongo wa mawazo uliniandama, niliikumbuka sana familia yangu, kuna wakati hadi nilikuwa ninaumwa kila nikiwakumbuka wazazi wangu, bibi yangu mwenye umri wa miaka 72 na ndugu zangu wengine, nimelia kwa muda mrefu sana, sijaweza kuwasiliana nao kwa muda mrefi hadi hivi karibuni nilipoanza kuongea nao kwa WhatsApp.
"Vita ni mbaya sana, watu wanafikiri Ukraine ni mji mdogo, lakini ni nchi yenye watu zaidi ya milioni 43.8, lakini tumevamiwa na kuharibiwa maisha yetu na nchi yenye watu zaidi ya milioni 143.4, athari ni kubwa sana hasa tukizingatia watu wengi hawana hati za kusafiria," anasema.
Vladyslava anasema alitua visiwani Zanzibar kwa ajili ya mapumziko lakini alishindwa kurejea Ukraine kutokana na vita hiyo, akalazimika kujifunza maisha ya wenyeji, akipokewa na raia wa Ujerumani ambao aliishi nao kwa muda baadaye akaamua kwenda kuishi kwake kwenye nyumba ya matofali ya udongo aliyojenga.
"Ninayafurahia maisha ya hapa kwangu, kwa sasa Ukraine hali ya hewa ni nyuzi joto sita hadi 12, kuna baridi kali sana pia chakula ni cha shida kutokana na vita. Hapa (Zanzibar) nina uhakika wa maisha, watu wanaishi maisha ya kawaida sana lakini ya amani, ninapata chakula, nimelima mapapai nimevuna.
"Hali ya Ukraine ni ngumu sana, watu hawana chakula, mali zimeharibiwa, wengi wako nyumbani hawana uhakika wa maisha. Kuishi hapa Zanzibar kuna ahueni kubwa ingawa muda wote mawazo ni kwa familia yangu.
"Ninapenda hali ya hewa ya hapa, nilikuwa sijui kupika lakini sasa ninapika, tena kwa gesi ya kawaida, sikuwahi kufua kwa mikono, nilifua kwa mashine, sikutarajia nitaishi kwenye nyumba isiyo na umeme wala maji na miundombinu ya kisasa.
"Nilikuwa sijui kutafuta maji lakini sasa ninatafuta maji, ninaishi maisha ya Kiafrika. Kuna wakati ninapitia maisha magumu sana, sina kipato chochote, ninasaidiwa na majirani, ninachofurahia ni amani niliyonayo, sisikii sauti za mabomu," anasema.
Vladyslava anainyoshea kidole Russia kwa anachokiita kuharibu kwa makusudi maisha ya zaidi ya watu milioni 43, akiitaja familia yake kwamba mdogo wake mwenye umri wa miaka 15 sasa anaishi Uswisi kama mkimbizi.
KUNUNUA NYUMBA
Binti huyo anasimulia maisha yake kwamba mwaka 2020 aliingia nchini kwa ajili ya likizo na kusherehekea siku yake ya kuzaliwa na alipapenda Zanzibar na kumwambia baba yake ambaye alimruhusu anunue ardhi.
Alirejea Zanzibar kwa ajili ya likizo nyingine Februari mwaka huu na wakati anajiandaa kuondoka, wakapata taarifa, Russia imeivamia kivita nchi yao.
"Niliwasiliana na baba aliniambia yeye atabaki Ukraine kupigania nchi yetu. Aliniambia nibaki Zanzibar, nisirudi Ukraine kutokana na hali iliyoko, haikuwa rahisi kwangu, tangu Februari hadi Juni nilikuwa ninalia tu kila siku, nimepoteza kila kitu kuanzia nyumba niliyokuwa nimepanga na ofisi ya kampuni yangu, sina ndugu hapa nilipo ila nina Watanzania ambao wamekuwa watu wema kwangu muda wote," anasema.
Vladyslava anasema majirani wanampenda, hasa watoto ambao wakitoka shuleni wanakwenda nyumbani kwake kuongea naye.
"Ninapenda sana watoto hadi ninafikiria baadaye nifungue kituo cha kulea watoto, nina marafiki wengi na ninajulikana," anasema.
Vladyslava anabainisha kuwa alipokuwa Ukraine, alikuwa anaishi maisha yake mwenyewe mbali na wazazi wake na alifungua kampuni inayotoa ushauri wa kibiashara na ujasiriamali na kumpatia fedha nyingi.
"Nilifungua kampuni nikiwa na miaka 19, ilikuwa inafanya vizuri sana, nilipata fedha nyingi lakini kutokana na vita biashara yangu iliharibika yote, nilikuwa na ndoto kubwa sana," anasema.
APATA MCHUMBA
Vladyslava anasema amepata mchumba ambaye ni Mzanzibar na amemwomba wafunge ndoa, lakini anafikiria kama yuko tayari kuishi maisha ya familia na kuwa na watoto.
"Ameniomba anioe ila bado ninafikiria kwa maisha niliyonayo ninaweza kulea mtoto? Watoto wana mahitaji mengi sana, ni lazima nijiandae kuwasaidia ipasavyo, ni lazima nifikirie kwa kina kabla ya kuwa na familia, ni uamuzi mgumu ambao lazima niufanye kwa uangalifu.
"Tumeshaongea, tumebaki kuwa marafiki wakati ninaendelea kutafakari uamuzi wangu, ameniambia anasubiri niamue," anasema Vladyslava na kusita kutaja jina la kijana huyo.
MAJIRANI WANENA
Ibrahim Rashid, jirani wa Vladyslava, anasema kuwa kijijini kwao ni umbali wa zaidi ya saa moja kutoka mjini Unguja na walimpokea raia huyo na kuishi naye kwa kumsaidia mahitaji ya msingi kutokana na nyumba yake kutokuwa vizuri.
"Awali ilikuwa vigumu sana kuishi naye, alikuwa na msongo wa mawazo, ilikuwa kazi kuzoea watu wengine na hasa maisha yetu haya, nilimsaidia kutafuta mafundi waelewa kujenga kibanda chake kwa kuwa kuna wakati ana fedha na wakati mwingine hana.
"Siku nyingine alikuwa anakuja kuishi kwangu, anataka kuchaji simu zake, lugha haikuwa shida sana kwa sababu nami shughuli zangu ni za utalii, hivyo ninaijua kiasi.
"Nilimpa mtungi wa gesi na mahitaji mengine, siku ninacho namsaidia, siku sina ninamwambia leo sina," anasema Rashid na kubainisha kuwa jirani yake huyo alipanga kujenga jengo la hadhi kubwa lakini akaamua kujenga kibanda kutokana na kukosa fedha.
Mmoja ya wanakijiji wa Kizimkazi, Hassan Ali anasema wanaishi vizuri na Vladyslava na kumwelezea kama binti anayependa kujichanganya na wanakijiji.
Mkurugenzi Uratibu wa Shughuli za Utalii kutoka Kamisheni ya Utalii Zanzibar, Omar Suleiman Mohammed anasema kulikuwa na raia wa Ukraine 1,200 waliokuja kwa shughuli za utalii ambao wakati vita vinatokea nchini mwao walikuwa visiwani Zanzibar.
Mohammed afafanua kuwa wakati vita vinaendelea, wengi wao waliondoka na kuelekea mataifa mbalimbali ya Ulaya kwa gharama zao, sita walisaidiwa usafiri na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) na 12 wamebaki Zanzibar.
"Kati ya hao 12, wapo waliokodi nyumba na wengine wamepewa hifadhi na serikali inawasaidia gharama za viza ili kuendelea kubaki nchini," anasema.
Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa (UN), vita vya Ukraine na Russia vilivyoanza Februari mwaka huu, vimesababisha zaidi ya raia milioni 6.3 kuikimbia Ukraine