RAIS Samia Suluhu Hassan ametoa muda wa mwaka mmoja (2023) kwa Waziri wa Nishati, Januari Makamba kuhakikisha taasisi zote kubwa nchini ikiwamo magereza na jeshi, zinasitisha matumizi nishati chafu ‘kuni na mkaa’ kupikia badala yake zihamie kwenye matumizi ya nishati safi ya kupikia. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Rais Samia, ametoa agizo hilo leo tarehe 1 Novemba, 2022 wakati akizundua mjadala wa Kitaifa wa Nishati safi ya kupikia, unaofanyika katika ukumbi wa Julius Nyerere International Convention Centre (JNICC), jijini Dar es Salaam.
Amesema ana bahati na Makamba kwenye mambo ya mazingira kwani akiwa Makamu wa Rais, alimuelekeza kuhakikisha taasisi zinazohudumia zaidi ya watu 300, lazima watumie nishati safi ya kupikia.
“Akiwa kule hakukaa muda mrefu akatoka hatukulitekeleza sasa nakuelekeza tena leo lilelile kwamba taasisi zile za Magereza, shule, vikosi vya ulinzi zianze sasa kujielekeza kwenye nishati safi ya kupikia.
“Sasa hivi sihesabu, maana mpo mwishoni mwishoni mkishughulikia mambo mengi ila mwaka mzima wa 2023 nataka mjielekeze kwenye hili la taasisi kubwa kutumia nishati safi ili 2024 nikirudi niwaambie Wananchi ni hatua gani nimefikia na nini nilifanya,” amesema.
Aidha, amesema ni lazima kutumia nishati safi ya kupikia kwa maendeleo ya nchi, jamii, na haki za wanawake.
“Wanawake wana mambo mengi ya kujitolea kazi zao bila malipo. Tumeona akina mama wanasonga ugali huku machozi yanawatoka. nani kamlipa? kapata fidia gani? pengine watoto hawamtunzi. Akina mama wa aina hii wapo wengi sana na hawalipwi angalau tuwapunguzie athari wanazozipata,” amesema.
Mjadala huo wa Kitaifa wa Nishati Safi ya Kupikia, unaofanyika kwa muda wa siku mbili (Jumanne Novemba 1-2, 2022), jijini Dar es Salaam umehudhuriwa na wadau mbalimbali wa nishati zaidi ya 3000 kwa malengo ya kujadili namna ya kumtua mama mzigo wa kuni kichwani.