Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania ‘TFF’ Wallace Karia amesema anakubali na kupokea lawama zote zinazoelekezwa kwake kuhusu mwenendo mzuri na mbaya wa Soka.
Rais Karia ametoa kauli hiyo leo Jumatano (Novemba 02), alipozungumza na Waandishi wa Habari jijini Dar es salaam, wakati wa hafla ya kusaini mkataba ba Kampuni ya Ndege ya Precision Air.
Kiongozi huyo amesema kwa muda alioongoza Soka la Tanzania kama Rais amekua akiona na kusikia lawama nyingi za nzito zinazoelekezwa kwake, kwa madai ya kulichukia kundi fulani na kulipendelea lingine.
Amesema mengi anayohusishwa nayo katika lawama hizo wala hausiki, lakini kwa mapenzi na chuki za wanaovumisha uzushi huo, wameamua kumchafua kupitia Mitandao ya Kijamii na katika baadhi ya Vyombo vya Habari.
“Nakubali kulaumiwa hata kwa mambo AMBAYO SIHUSIKI. Kuna wakati nalaumiwa kuhusu hukumu za kamati ya saa 72 ambazo hata sihusiki.”
“Siku nitakapokaa pembeni MTANIKUMBUKA… Nami sitakufa mapema nitakuwa nimekaa nawatazama”
“Nawatakia kila la kheri timu zote za Tanzania zinazocheza michuano ya kimataifa, nawaombea washinde katika mechi hizo.” amesema Wallace Karia.
Kiongozi huyo aliingia madarakani mwaka 2017, akirithi kijiti cha Urais wa TFF kutoka kwa aliyemtangulia Jamal Malinzi aliyeoongoza kwa kipindi kimoja kuanzia mwaka 2013.