Waimbaji nyota wa muziki nchini, @officialkilly_tz na @officialcheed sasa ni rasmi wapo huru. Wote wawili wamethibitisha hilo kupitia insta story zao na wameeleza ni wakati sasa wa kuwapa mashabiki wao kile wanachostahili.
Kauli hiyo ya kuwa huru iliyotolewa na Cheed pamoja na Killy ni kufuatia Harmonize jana Jumanne katika ofisi za Baraza la Sanaa la Taifa (Basata) kuvunja mkataba rasmi kimaandishi na waliokuwa wasanii wake Killy na Cheed.
Kwa mujibu wa gazeti la Mwananchi ambao wao walipata exclusive interview na meneja wa kina Cheed, Saty Sembe ambaye ameliambia gazeti hilo kuwa, kikubwa walichokuwa wanakipigania Killy na Cheed ni kupewa barua ya kimaandishi ili kuwa huru kufanya kazi zao ikiwemo kuweza kuingia mikataba na watu wengine.
Jambo la pili Sembe ameliambia Mwananchi kwamba, Killy na Cheed walikuwa wanapigania kuachiwa kwa kurasa za mitandao yao ya kijamii ambayo ni moja ya chanzo cha kuwaingizia hela kwa kuuza kazi zao. Kuhusu kulipwa Sh10 milioni kila mmoja na Konde Music wanayotakiwa kulipwa, Meneja huyo amesema watalipwa hata baadaye.
Itakumbukwa, Cheed na Killy walijiunga rasmi na lebo ya Konde Music Worldwide, Septemba 2020 wakitokea lebo ya King’s Music inayomilikiwa na msanii AliKiba.