Mbunge wa Morogoro Kusini Mashariki #BabuTale na Meneja wa Msanii #DiamondPlatnumz lakini pia mmoja wa wakurugenzi wa kampuni inayojihusisha na shughuli za burudani, Tip Top Connections Company Limited yuko hatarini kufungwa jela kutokana na kushindwa kumlipa mhadhiri wa dini ya Kiislam, Sheikh Hashim Mbonde, fidia ya Sh250 milioni.
Tayari #SheikhMbonde ameshafungua maombi Mahakama Kuu akiiomba mahakama hiyo iamuru #BabuTale akamatwe na afungwe kwa kushindwa kumlipa fidia hiyo.
#SheikhMbonde amefungua maombi hayo dhidi ya Tip Top na Babu Tale baada ya Mahakama ya Rufani kutupilia mbali taarifa yao ya kusudio la kukata rufaa kupinga hukumu ya Mahakama Kuu iliyowaamuru kulipa fidia hiyo, Agosti 17, 2022.
Katika kesi ya msingi, Sheikh Mbonde alikuwa akidai kuwa aliingia mkataba na kampuni ya kina Babu Tale (Tiptop Connection) ili wamrekodi mahubiri yake kisha wayauze na kugawana mapato.
Hata hivyo baada ya kurekodi masomo saba, walimkatia mawasiliano na alipowatafuta na kukutana nao wakamweleza kuwa wameamua kuachana na mpango huo.
Sheikh Mbonde alidai kuwa akiwa kwenye mahubiri Dodoma ndipo akakutana na mikanda ya video katika mfumo wa DVD yenye mahubiri yake huku kukiwa na namba za simu za viongozi hao wa Tiptop.
Sheikh Mbonde alidai baada ya kufanya uchunguzi alibaini kuwa DVD hizo zilikuwa zikiuzwa katika mikoa mbalimbali, ndipo akawafungulia kesi ya madai ya fidia kutokana ukiukwaji wa Sheria ya Hakimiliki na Hakishiriki.
Baada ya kupeleka madai yake Mahakamani, Mahakama ilimuamuru Babu Tale kumlipa Mhadhiri wa Dini ya Kiislamu, Sheikh Hashim Mbonde kiasi cha Sh250 milioni, baada ya kupatikana na makosa ya ukiukwaji wa haki za hakimiliki kwa kutumia masomo yake kibiashara bila ridhaa yake kinyume cha Sheria ya Hakimiliki na Hakishiriki.
Source: Rickmedia/Bongo5