WOTE tulikuwa tunafahamu kuwa kilichokuwa kinamuweka nje ya uwanja kwa muda beki wa kulia wa Simba, Shomari Kapombe ni majeraha, lakini kumbe ilikuwa ni tofauti ya tulichokuwa tunakifahamu.
Kapombe amefunguka kwa mara ya kwanza baada ya kurejea uwanjani akisema kuwa ni kweli alikuwa nje ya uwanja akiwa mgonjwa, lakini kwa bahati mbaya hakuwahi kujua anaumwa nini kwani hata madaktari walishindwa kugundua kilichokuwa kinamsumbua.
Kapombe alisema alikuwa hayupo sawa kwenye mwili wake akijiona kabisa anaumwa, lakini kila alipokwenda hospitali kufanyiwa vipimo, ugonjwa uliokuwa unamsumbua haukuwahi kuonekana.
“Kweli nilikuwa nje ya uwanja nikiwa najiona kabisa kuwa mimi ni mgonjwa na mwili wangu haupo sawa. Lakini kwa bahati mbaya kila nilipokuwa naenda hospitali kupima madaktari walikuwa hawaoni ugonjwa.
“Ilikuwa inaniumiza sana kwa sababu mimi nina familia ambayo inanitegemea kupitia kazi yangu ya mpira. Ukitazama timu yangu pia ilikuwa inahitaji mchango wangu. Nashukuru Mungu kwa sasa niko sawa na nguvu yangu imerejea kama kawaida,” alisema Kapombe.
Kapombe alikosa mechi za Simba tangu alipoumia kwenye mchezo wa timu hiyo dhidi ya Tanzania Prisons, kabla ya kurejea hivi karibuni na kuichezea timu hiyo kwenye mechi dhidi ya Mtibwa Sugar na Ihefu kwenye Dimba la Mkapa na ile ya ugenini mbele ya Singida Big Stars.