KOCHA Mkuu wa Singida Big Stars, Hans van Pluijm, amesema wamezisoma mbinu za Yanga na wako tayari kuvunja rekodi yao ya kutofungwa 'Unbeaten', kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara watakapokutana kesho katika Uwanja wa Benjamin Mkapa.
Akizungumza na gazeti hili jana, Pluijm alisema maandalizi yanaendelea vizuri na wachezaji wake wako tayari kwa ajili ya mchezo huo kwa kucheza kwa tahadhari kubwa ili kuvunja rekodi ya Yanga.
Alisema amewasoma na kufahamu ubora wa wapinzani wao hao, hivyo anaamini mchezo utakuwa mgumu kwa sababu wanahitaji kupata matokeo chanya na Yanga wakitaka kuendelea kulinda rekodi yao ya kutopoteza.
"Nimewasoma Yanga vizuri, ina wachezaji wazuri na mabingwa watetezi, lakini wanarekodi yao ya kutofungwa, kwa maandalizi ya timu yangu na ubora tulionao ninaimani kitaleta ushindani mkubwa.
"Kuhusu kuvunja rekodi ninaamini inawekezana kwa sababu ya maandalizi tunayofanya kuelekea mchezo wetu dhidi ya Yanga," alisema Pluijm.
Alisema malengo yao makubwa ni kufanya vizuri kwenye mchezo huo ili kupata pointi tatu kwa ajili ya kufikia malengo yao ya kuendelea kupanda katika nafasi za juu kwenye msimamo.
Singida Big Stars watashuka dimbani kesho majira ya saa 1:00 usiku kusaka pointi tatu ili kuendelea kujiweka katika nne bora, wakati huu ikiwa katika nafasi ya nne na alama 18 baada ya kushuka dimbani mara 10 hadi sasa kwenye ligi hiyo.
Licha ya kucheza mechi pungufu tofauti na timu nyingine za ligi hiyo, Yanga ipo kileleni mwa msimamo ikiwa na pointi 23 baada ya kushuka dimbani mara tisa na haijapoteza mechi yoyote tangu msimu uliopita hadi sasa.