UNAAMBIWA Yanga ina jambo lake katika jezi rangi nyeusi inayopenda kuitumia na kuivaa sana kwa sasa katika mechi zake.
Jezi hiyo ina mzuka wa aina yake na haijawahi kuiangusha pindi inapocheza mchezo wowote.
Ni kama ina bahati Fulani hivi kwa mabingwa hao wa kistoria wa Ligi Kuu kwa mwaka huu tangu ilipoivaa na kumtoa Mwarabu wa Tunisia ugenini na kufuzu hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho la Afrika.
Rasmi Yanga ilianza kuivaa jezi rangi nyeusi Oktoba 26, dhidi ya KMC kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam na kuibuka na ushindi wa bao 1-0 lililofungwa na Feisal Salum ‘Fei Toto’.
Ikiwa katika hali ngumu baada ya kutoka sare tasa nyumbani dhidi ya Club Africain ya Tunisia katika mchezo wa kufuzu hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho, Novemba 9, Yanga ilitinga uzi huo nchini Tunisia na kuibuka na ushindi wa bao 1-0 katika Uwanja wa Hammedi Agrebi Olympic ambao zamani ulikuwa ukiitwa 7 Novembre.
Lilikuwa ni bao la ugenini la Mburkinabe, Stephan Aziz Ki lililotosha kuwavusha mabingwa hao wa kihistoria wa Ligi Kuu Tanzania katika hatua hiyo.
Yanga ambayo imejitambulisha zaidi kwa kuvaa jezi zenye rangi ya asili za kijani na njano baada ya kuitoa Club Africain imeonekana kunogewa zaidi na uzi huo mweusi kwani Novemba 13, iliuvaa tena na kupata ushindi dhidi ya Kagera Sugar katika Uwanja wa Kirumba.
Bao la straika kinda, Clement Mzize lilitosha kuipa klabu pointi tatu muhimu katika Ligi Kuu.
Kama haitoshi, Novemba 17, Yanga ilishusha kipigo kitakatifu dhidi ya Singida Big Stars (BSS) ikiwa ndani ya uzi mweusi.
Straika Fiston Mayele aliondoka na mpira baada ya kufunga mabao matatu ëhat trickà na beki Kibwana Shomary akitoka na bao lake la kwanza.
Mara baada ya mchezo huo wa Ligi Kuu kumalizika Msemaji wa Yanga, Ally Kamwe aliposti picha ya kikosi cha timu hiyo kikiwa kimevaa uzi mweusi kwenye mitandao na kuandika maneno yaliyosomeka ‘Rais naomba hizi jezi nyeusi tusizivae tena tutakuja kuua watu’ na Rais wa Yanga, Said Hersi alikomenti kwa kuonyesha imoji za kucheka.
Rais Hersi, alipouzwa kuhusu jezi nyeusi za Yanga na matokeo wanayotapata alisema jezi ya rangi hiyo ndiyo pendwa kuanzia kwa mashabiki hadi wachezaji wa Yanga na kudai ndio jezi inayoongoza kwa kufanya vizuri katika mauzo, lakini hakutaka kusema kama ni jezi ya bahati au la kwa upande wao.
“Siku chache baada ya kuzinduliwa na kuingizwa sokoni iliongoza kwa mauzo sokoni. Hadi sasa bado inafanya vizuri sana, alisema na kuongeza:
ìKuhusu kuvaliwa na timu na kupata matokeo sina jibu la moja kwa moja japokuwa naamini ni imani tu kwa sababu jezi haichezi.”
MSIKIE FEI TOTO
Mwanaspoti lilizungumza na kiungo wa Yanga, Feisal Salum kuhusu jezi hiyo naye alisema hawaamini kama rangi hiyo ya jezi inawapa matokeo ila imewajengea ari ya kupambana uwanjani.
“Sio kweli kuvaa jezi rangi nyeusi tu tunaweza kupata matokeo. Ni lazima tupambane na kufanya yale yatakayotupa ushindi,” alisema Fei Toto na kuongeza;
“Jezi hazichezi ila tumekuwa na ari ya ushindani kwa sababu zimetupa nguvu (mzuka) tangu tumetoka Tunisia, ukifuatilia mechi zote ugenini na nyumbani tumevaa uzi mweusi.”
CHUKUA HII
Imani katika jezi ipo katika timu nyingi duniani. Aprili 13, 1996 Manchester United ya Ligi Kuu England ikiwa chini ya kocha wake, Alex Ferguson ikicheza dhidi ya Southampton mpaka kufikia mapumziko katika Uwanja wa The Dell (sasa Saint MaryÃs), ilishafungwa mabao 3-0 katika kipindi cha pili United ilibadilisha jezi za kijivu iliyokuwa imezivaa.
Ferguson akiwa mwenye hasira alidai wachezaji wake walikuwa hawawezi kuonana vizuri kwenye mwanga mkali wa jua kutokana na rangi ya jezi hizo.
Man United ilibadilisha jezi hizo na kuvaa za rangi ya bluu na nyeupe, hadi mwisho mchezo uliisha kwa miamba hiyo kupoteza kwa mabao 3-1.