Sugu Adai Katiba Mpya itampa Heshima Rais Samia



Mbunge wa zamani wa Jimbo la Mbeya Mjini kwa tiketi ya CHADEMA, Joseph Mbilinyi maarufu kama Sugu, ameshauri uarakishwaji wa upatikanaji wa katiba mpya huku akidai kitendo hicho kitampa heshima kubwa Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan 



Mwanasiasa huyo ametoa ushauri huo alipozungumza kwenye Mkutano Mkuu wa Chadema Jimbo la Tarime Vijijini mkoani Mara, ambapo amesema maamuzi hayo yataweka historia njema ya utumishi wa Rais atakapoondoka madarakani


“Na tunaendelea kushauri, kwa sababu unapokuwa kiongozi lazima uwe na dream (ndoto) uwe na ile ari ya kuacha regency (Utawala). Kwa hiyo Mhe Rais Samia anayo nafasi ya kuacha regency, aiache hii nchi na Katiba Mpya kwa sababu ndiyo takwa la wananchi na itamfanya aondoke vizuri, awe Rais mstaafu mzuri,” amesema Sugu.


Kwa upande wao, Wajumbe wa Kamati Kuu ya chama hicho cha upinzani, John Heche, Ezekiel Wenje, Peter Msigwa na Gimbi Dotto Masaba, wameishauri pia Serikali kuongeza uwajibikaji katika ujenzi wa maendeleo ya watu na kuondoa vikwazo vya kisiasa.


“Tunataka Serikali ifanye wajibu wake wa maendeleo, ndiyo maana sisi tunalipa kodi. Tunaelewana vizuri? Wewe useme nifanyekazi mbili nilipe kodi wakati huo nijenge choo, Tarime haitaruhusiwa hiyo kitu. Kazi ya mwananchi alipe kodi Serikali ifanyekazi ya maendeleo. Na kazi ya maendeleo siyo hisani,” amesema Heche.


“(Kupanda) Bei ya unga, bei ya sukari, bei ya bando, bei sijui ya nini, kuvuta ndege kwa kamba, hakuna maji, hakuna umeme. Nendeni (Wana Chadema) mkajenge chama, tufanyekazi, tujipange Uchaguzi wa Serikali za Mitaa ndiyo kipimo cha kwanza, hawa watu (CCM) hawawezi kutushinda, les go a oncy (twende sawa)” Wenje amesema.


“Hii nchi siyo mali ya CCM mnajua au bado? Hii nchi ni ya Watanzania wote. Nchi hii ni ya mfumo wa vyama vingi, tunapaswa tushindane kwa sera,” amesema Mchungaji Peter Msigwa.


“Fanyeni michakato yote lakini mhakikishe kundi la wanawake hamjaliacha nyuma. Gombeeni (Wanawake) nafasi za uongozi na hasa kwenye nafasi za maamuzi,” amesema Gimbi Masaba.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad