YANGA ilirejea jana mchana saa 8 mchana, ikitokea Tunisia ilipoweka rekodi kubwa ya kushinda mechi ya CAF katika ardhi ya Uarabuni. Kiungo aliyechangia kwa kiasi kikubwa kuukamata mchezo huo wa Club Africain kiufundi, Salum Aboubakar ‘Sure Boy’ amefichua siri ya ushindi.
Akizungumza kwa njia ya simu na Mwanaspoti, Sure Boy alisema wakati alipoitwa kwa mara ya kwanza na kocha wake Nasreddine Nabi kumueleza anataka kumpa nafasi ya kuanza hakushtuka ila alijisemea rohoni hiyo ndio gia yake ya kuanza kuiteka nafasi kwenye kikosi cha kwanza.
Sure Boy alisema alijipanga kuhakikisha anafanya kila kitu ambacho kocha wake anakitaka kiufundi na kujikuta anakuwa na kazi rahisi kuwabana Club Africain katikati ya uwanja na mashabiki wao kuishia kusonya na kuvuta sigara kwa wingi.
“Nilipokaa na kocha mara ya kwanza tu hesabu zangu zilianzia hapo nikajisemea moyoni hakuna nafasi nyingine, hii inatosha kuonyesha umuhimu wangu kwanini nipo Yanga,” alisema Sure Boy ambaye ni staa wa zamani wa Azam FC na Friends Rangers za Dar.
“Nilikuwa na mambo mawili kichwani, kwanza kutekeleza yale ambayo kocha ametaka niyafanye lakini la pili kuisaidia timu kufikia malengo kwa kufuzu hatua inayofuata, tuliona timu yetu na mashabiki hawastahili machungu ya kutolewa tena tukaazimia kama wachezaji,”aliongeza mchezaji huyo ambaye baba yake alicheza Yanga kama winga.
Alisema kuwa haikuwa kazi ngumu kwake kuonyesha ubora wa kupiga pasi na kuziunganisha idara mbili za ushambuliaji na kiungo na sasa wanajipanga kuhakikisha wanatumia morali ya ushindi huo kurudisha heshima yao ya kuendelea kushinda.
“Hii ni kazi yangu, kiwango nilichokionyesha siwezi kusema ni kitu kikubwa sana labda kwa sababu sikuwa hapa Yanga kwa muda mrefu lakini watu wataona makubwa zaidi ya hiki ambacho nimekionyesha,” alisema
“Mimi kupiga pasi ni kazi yangu nashukuru niliusambaza upendo kwa kila mmoja aliyeutaka (kupiga pasi zilizofika) lakini kitu kikubwa hapa tumemaliza mechi hii tunatakiwa kama wachezaji kutambua hii ni nafasi ya kubadilisha upepo mbaya uliokuwa unapita.
“Sasa tunakwenda mbele kushinda mataji mengine na mechi zinazokuja tukitumia morali kama hii, tunaamini wananchi nao wametusamehe, hivyo nao warudi uwanjani tushirikiane kuipa nguvu timu yetu,”alisema kwa kujiamini.
RAMANI ILIYOCHORWA HIVI
Habari kutoka ndani ya Yanga zinasema Nabi aliwaambia viongozi wamuachie afanye kazi yake kwenye nchi yake ya Tunisia.
Alichofanya akapanga kambi ianzie Mji wa Sousse walipokaa kwa siku tatu. Akiwa huko akacheza akili na mtandao wake wa watu wa mpira akapata mbinu zote za wenyeji na jinsi ya kuwakabili ikiwemo kwa wapinzani wa Africain ambao ni Etoile du Sahel.
Etoile waliwapa kila kitu Yanga juu ya siri za wapinzani wao huku pia Club Africain wakihofia kufika mji huo wakitambua ni rahisi kwao kugundulika kutokana na uwepo wa makocha watatu wa Yanga ambao wanawajua vizuri.
Ukiacha na Nabi Yanga ina kocha wa mazoezi ya viungo Helmy Gueldich na daktari wa viungo, Youssef Mohamed ambao mara kwa mara walikuwa wanapokea taarifa nyingi za wapinzani wao na kuzifanyia kazi. Taarifa za ndani kabisa ni kwamba uongozi umetumia zaidi ya Sh200 milioni kama maandalizi ya mchezo huo ugenini. Kambini walibadili pia utaratibu wa kutumia vyakula maalumu kwa kujipikia badala yake walichimba mkwara kwa wamiliki wa hoteli hizo na wakapata chakula kinachotumiwa na wageni wote waliokuwa wamepanga.
Yanga waliambiwa na Etoile mpaka milango ya kuzingatia kuingia uwanjani, jambo lililowashtua wenyeji.
KIKAO CHA WACHEZAJI
Walikaa kikao cha dakika 35 chini ya Rais wao, Hersi Said na kuambiana ukweli kwenye mambo ya msingi ikiwemo uwajibikaji uwanjani, upendo, malengo pamoja na ushirikiano.
“Alikuwa mkali sana na akatuambia hakuna mtu wa Yanga anayetaka kusikia kitu kingine zaidi ya ushindi katika mechi ya jana (juzi) na sote sisi ni wachezaji wa Yanga tuache kupigana majungu na kucheza kwa kufikiria sifa binafsi, unajua ushindi ni wa timu kwahiyo kile kikao kilisaidia sana hasa pale aliposema kama tukitolewa tusilaumiane.
KIKOSI CHA KWANZA
Habari za ndani zinasema kwenye kikao cha makocha na viongozi na baadhi ya wachezaji waandamizi walipewa nafasi ya kushauri juu ya kikosi na kutaka Aziz Ki aanzie benchi jambo ambalo lilizaa matunda alipoingia kuchukua nafasi ya Khalid Aucho.
Lakini Nabi akawasisitiza wachezaji kwamba kikichafuka uwanjani au wakipoteza shepu yao warudishe mpira haraka kwa kipa Diarra atoe maelekezo na uelekeo wa kiufundi. Yanga imefuzu hatua hiyo ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika kwa mara ya tatu.