WAKATI ladha za Ligi Kuu Bara zikiendelea kwa kila timu kujitafuta ili kufikia malengo yake, vita imehamia kwenye kuwania kiatu cha ufungaji bora ambapo mastaa wa 10 wameonesha kuwania tuzo hiyo.
Hadi sasa mbio za kuwania kiatu hicho, zinaongozwa na winga wa Mbeya City, Sixtus Sabilo mwenye mabao saba huku mastaa wengine tisa wakimfuata.
Moses Phiri wa Simba, Fiston Mayele (Yanga), Idriss Mbombo (Azam FC) na Reliants Lusajo (Namungo fc) wakifuatia kila mmoja akiwa na mabao sita.
Wengine walio kwenye 10 bora ya mastaa wanaowania kiatu hicho ni Feisal Salum (Yanga), Moubarack Amza (Coastal Union), Anuary Jabir (Kagera Sugar), Matheo Antony (KMC) na Abalkassim Suleiman (Ruvu Shooting) kila mmoja akiwa na mabao manne.
Katika orodha hiyo wachezaji wanne tu, Mayele (16), Lusajo (10) Matheo (9) na Anuari aliyekuwa na mabao saba ndio walikuwa kwenye 10 bora ya wafungaji bora wa msimu uliopita ambapo George Mpole aliongoza kwa kufunga mabao 17.
Sabilo ambaye ni kinara hadi sasa, aliliambia Mwanaspoti kuwa kipaumbele chake zaidi msimu huu sio kiatu cha ufungaji bora bali ni kutoa asisti zaidi akiwa nazo tano hadi sasa.
“Nafurahi kufunga lakini sio kipaumbele changu, lengo ni kuifanya timu ifikie malengo na mimi binafsi natamani niwe na namba nzuri kwenye kuasisti lakini kila nikipata nafasi ya kufunga nitafanya hivyo,” alisema.