Waliofariki Ajalini Dodoma Watambuliwa



WATU sita wamekufa wakati basi la abiria lilipogongana na lori katika eneo la Mzakwe mkoani Dodoma.

Katika ajali hiyo, basi la Arusha Express lenye namba za usajili T530 AGG liligongana na lori la mchanga la kampuni ya Sinohydro, lenye namba za usajili T939 DZE jana, saa sita mchana.

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule alisema akiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma kuwa majeruhi 22 walipelekwa katika hospitali hiyo wakiwamo wanawake 10 na wanaume ni 12.

“Niwashukuru sana watu wote walioshiriki kuwaokoa na kutoa huduma ya kwanza na wataalamu wetu wa afya ambao wanaendelea kuwahudumia,” alisema Senyamule.


Alihimiza wanaoendesha vyombo vya moto wawe makini kwa kuwa ajali hiyo imetokea kwenye eneo lililonyooka.

“Lakini inasemekana wenzetu wa lori walikuwa wana-overtake sehemu ambayo haikuwa sahihi na kusababisha ajali ambayo imesababisha Watanzania sita kupoteza maisha na majeruhi ambao tunaomba Mungu aendelee kuwapa afya njema na uponyaji wa haraka,” alisema Senyamule na akaomba wananchi wajitokeze kuchangia damu.

Aliwashukuru watumishi wa afya kwa kazi wanayoendelea kuifanya kuokoa maisha ya waliojeruhiwa na kwamba wanaifanya kazi hiyo kwa uamunifu, juhudi na weledi.


Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mkoa wa Dodoma, Dk Ibenzi Ernest alisema miili ya watu sita waliokufa kwenye ajali hiyo walipokelewa hospitalini hapo.

“Tunaendelea kuwapitia huduma majeruhi na hali zao zinaendelea vizuri. Nitoe wito kwa watumiaji wa vyombo vya moto kuendelea kuchukua tahadhari kuepusha ajali. Serikali imekuwa ikitumia gharama kubwa kuwatibu majeruhi, tunapokinga kwetu watumiaji wa barabara inakuwa ni nafuu sana,” alisema Dk Ernest.

Aliwataja marehemu waliotambuliwa kuwa ni Kurwa Awadhi ambaye ni dereva wa basi, Amani Athumani, Yohana Paulo na Humphrey Mdoe ambao walikuwa ni mawakala wa basi hilo.

Dk Ernest alisema marehemu wawili wanaume wanaokadiriwa kuwa na umri wa miaka 30 walikuwa hawajatambuliwa akiwemo dereva wa lori.


Mmoja wa majeruhi katika ajali hiyo, Nelson Kajolo alisema lori hilo lililipita gari lingine na kuligonga basi walimokuwa.

“Basi letu halikuwa kwenye mwendo mkali na dereva alijitahidi kukwepa lakini ikashindikana, tukagongana uso kwa uso,” alisema.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad