Wanafunzi wadaiwa kuingilia mfumo, waghushi malipo ada




ZAIDI ya wanafunzi 260 wa Chuo Kikuu cha Iringa wanadaiwa kuingilia mfumo wa chuo, ujulikanao kama SAMIS na kufanikiwa kujiorodhesha majina, hivyo kuonekana kama wamelipa ada.

chuo kikuu iringa.
Kwa kufanya hivyo, wanafunzi hao wanaonekana hawadaiwi, hivyo  kukikosesha chuo  mamilioni ya shilingi. Pia wanadaiwa kughushi stakabadhi za malipo na mihuri ya benki ili kujiridhisha kuwa hawadaiwi ada.

Uchunguzi wa kina ambao umefanywa na gazeti hili na kuthibitishwa na uongozi wa chuo, umebaini wanafunzi waliofanya hujuma hiyo ni wanaosomea cheti na shahada (bachelor) hali ambayo imeleta taharuki kubwa chuoni hapo.

Ada wanayopaswa kulipa wanafunzi wanaosomea cheti (certificate) kwa mwaka ni Sh. 840,000 wakati wa shahada mwaka wa kwanza ada yao ni Sh.1,670,400, mwaka wa pili Sh.1,610,400 na mwaka wa tatu ada ni Sh.1,760,400.

Mfumo wa SAMIS unaodaiwa kuingiliwa na wanafunzi hao unatumika na chuo hicho katika masuala ya malipo ya ada, kuweka kumbukumbu za wanafunzi na masomo.


Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Iringa, Prof. Ndelilio Urio, akizungumza katika mahojiano na gazeti hili, alikiri tatizo hilo kujitokeza katika chuo hicho na kwamba uongozi ulichukua hatua kuunda tume ya watu wanne ambao wanaendelea kuchunguza.

Alisema uchunguzi wa awali uliofanywa ulibaini wanafunzi 262 ndio walihusika katika kuingilia mfumo huo ambao baada ya kufanikiwa na ukaonyesha wamelipa ada, waliruhusiwa kufanya mitihani kabla chuo hakijashtukia hujuma hiyo.

Prof. Urio alipoulizwa inakuwaje wanafunzi waingilie mfumo wakati hawana 'saver’, alisema baadhi ya wanafunzi wanasomea masomo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), hivyo kuna uwezekano wa kufanya hujuma hizo.


Alisema mbali na kuingilia mfumo, pia wanafunzi wamebainika walikuwa wakighushi stakabadhi za malipo ya benki na mihuri ambazo nazo zilikuwa zikipelekwa chuo ili kujiridhisha kwamba wamelipa ada wakati si kweli.

Kutokana na hujuma hiyo ambayo alisema ilikuwa ikifanyika hata miaka ya nyuma lakini haikuwahi kubainika, alisema wanafunzi waliobainika wamepewa muda hadi Novemba 11, mwaka huu, wawe wamelipa ada.

"Baada ya kuwabaini wanafunzi waliofanya hujuma hiyo huku wakiwa tayari walishafanya mitihani, tumezuia matokeo yao hadi watakapolipa ada," alisema.

Alisema Novemba 22, mwaka huu Baraza la Chuo litakutana katika kikao kujadili suala hilo na kuona hatua gani zichukuliwe kwa wanafunzi ambao watakuwa hawajalipa ada.


Hata hivyo, alisema baadhi ya wanafunzi wanaodaiwa wameshaanza kulipa ada na hivyo chuo kimewapa matokeo ya mtihani walioufanya.

Kuhusu madai ya kwamba wanafunzi waliobainika kuingilia mfumo huo wananyanyaswa na askari wanaosoma chuoni hapo kwa kupigwa na kupelekwa polisi, alisema madai hayo si ya kweli bali yanaenezwa na watu wasiokitakia mema chuo hicho.

Prof. Urio alisema kuna askari na wanajeshi wanaosoma katika chuo hicho lakini kamwe chuo hakijawashirikisha katika sakata hilo.

Katika kukabiliana na tatizo lisijitokeze tena, alisema chuo kimeanza kuchukua hatua kwa kuwasiliana na Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT) kwa ajili ya kutengeneza mfumo mpya ambao utaunganisha chuo na benki moja kwa moja.


Rais wa Serikali ya Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Iringa, Hans Mejooli, alisema hujuma hizo zilibainika Agosti, mwaka huu, na baada ya hapo iliundwa timu ya kuchunguza zaidi suala hilo.

Alisema wanafunzi wanaodaiwa kuhusika na kuingilia mfumo huo wanasomea cheti na shahada ya kwanza na kwamba licha ya kufanya hujuma hizo, bado wako chuoni huku uchunguzi ukiendelea.

Kama  wazazi wa wanafunzi hao wamejulishwa suala hilo, alisema baadhi walijulishwa na kwamba wahusika ni wanafunzi wenyewe kwa kuwa walipewa pesa na wazazi wao.

Baadhi ya wazazi wa wanafunzi ambao wamehusika katika hujuma hiyo, wakizungumza na gazeti hili, walilalamika watoto wao kunyanyaswa kwa kuzuilia matokeo kwamba hawajalipa ada.

"Kama kuna hujuma ya kuingilia mfumo wa chuo mbona sisi kama wazazi hatujajulishwa suala hili na inakuwaje wanafunzi waingilie mfumo huu wakati 'saver' wanayo walimu? Hapa kuna jambo linajificha nyuma ya pazia," alisema mzazi mmoja ambaye aliomba jina lake lisitajwe.


Mzazi mwingine alihoji kama kuna hujuma kama hizo ni kwa nini uongozi wa chuo haujalifikisha suala hilo Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) ili kufanyiwa uchunguzi na kama mfumo huu una upungufu ufanyiwe maboresho ili kuondoa hujuma zaidi zisijitokeze.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad