Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limeazimia kuwa Wanafunzi wenye vigezo vya kupata mikopo ya elimu ya juu ambao hawajapata mikopo hiyo mpaka sasa Serikali iangalie namna ya kuwawezesha kupokelewa Vyuoni ili waendelee na masomo yao wakati Serikali ikitafuta fedha ya mkopo kwa ajili ya Wanafunzi hao.
Hatua hiyo imekuja baada ya Mbunge wa Biharamulo, Eng. Ezra Chilewesa kusimama na kuliomba Bunge kuahirisha shughuli zake zilizopangwa kwa muda ili kujadili tatizo la Wanafunzi kukosa mikopo ya elimu ya juu.
Hoja hiyo iliungwa mkono na Wabunge na Spikawa Bunge alitoa nafasi ya Wabunge kujadili na kutoa michango yao na hatimaye Bunge likaazimia Wanafunzi hao wawezeshwe kuendelea na masomo.
Kwa upande mwingine Spika wa Bunge, Dr. Tulia Ackson ameshangaa hoja ya Bodi ya Mikopo kudaiwa kumgomea Waziri mwenye dhamana kufanya kazi yake hivyo ameagiza Bodi hiyo kufika mbele ya kamati ya Bunge ya Huduma za Maendeleo ya Jamii November 04, 2022 ili kutoa maelezo kwanini Bodi ya Mikopo inagomea maelekezo ya Waziri wa Elimu.