Dar es Salaam. Abiria watano kati ya watu 19 waliofariki katika Ajali ya ndege ya shirika la ndege la Precision Air iliyotokea leo Novemba 6 Bukoba mkoani Kagera, ni watumishi wa Menejimenti na Maendeleo ya Afya (MDH).
Ajali hiyo imetokea leo Novemba 6 wakati ndege hiyo ikijaribu kutua katika uwanja wa ndege wa Bukoba, lakini kutokana hali ya hewa kuwa mbaya, ilipoteza mwelekeo na kutumbukia katika ziwa Victoria.
Mkurugenzi Mtendaji wa MDH, Dk David Sando amelithibitishia Mwananchi kuwa watumishi hao watano ni miongoni mwa wengine wanane wa ofisi hiyo waliokuwa safarini kwenda Bukoba.
“Watumishi wetu jumla walikuwa wanane na awali walitolewa watatu ambao hali zao hazikuwa nzuri wakapelekwa hospitali lakini baadaye waliweza kutolewa watano ambao hawakuweza kuishi, wamefariki,” ameelezea Dk Sando kwa masikitiko.
Ametaja majina ya watumishi waliopoteza maisha kuwa ni pamoja na watafiti watatu wakiwemo Dk Boniface Jullu, Dk Neema Faraja na Dk Alice Simwinga pamoja na Sauli Happymark pamoja na Mkuu wa kitengo cha mawasiliano MDH ZarchariaMlacha.
Amewataja watumishi watatu waliofanikiwa kuokolewa kuwa ni pamoja na Nickson Jackson, Dk Josephine Mwakisambwe na Dk Felix Otieno.
Dk Sando amesema wataalamu hao wa afya ya jamii walikuwa wakielekea Tabora wakipitia Mwanza na kwamba lengo la safari hiyo ilikuwa ni mkutano wa mwaka kwenda kuangalia maendeleo ya miradi.