Abiria walizwa Dar, Latra yaamuru nauli zilizoongezwa zirudishwe



Dar es Salaam. Wakati idadi ya abiria wanaosafiri kwenda mikoa mbalimbali na nchi jirani imeongezeka huku Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri Ardhini (Latra) imeamuru mabasi yalioongeza nauli kiholela kuwarudishia abiria.

Imekuwa ni kawaida kila ifikapo mwisho wa mwaka, mabasi yamekuwa yakioongeza nauli kinyume na utaratibu kutokana na ongezeko la abiria.

Akizungumza leo Ijumaa Desemba 23, 2022 wakati akifanya ukaguzi kwenye Stendi ya Magufuli Mbezi Luis jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa Latra, Habibu Suluo amewataka wasimamizi wa mabasi yaliyozidisha nauli kurudisha.

Miongoni mwa mabasi yaliyozidisha nauli ni kampuni ya Nazareti linalokwenda Iringa ambapo abiria wametozwa Sh35, 000 badala ya Sh 28,000.


Abiria Veronica Benjamin anesafiri kwenda Iringa amesema baada ya kufika kituoni hapo aliambiwa hakuna usafiri lakini baadaye aliambiwa kama ana Sh 35,000 usafiri upo.

"Kutokana na ongezeko la abiria, wanaokata tiketi wanapandisha nauli kwa kuwa wanajua lazima tusafiri, kama mimi nimelipa Sh 70,000 kwa watu wawili," amesema Veronica.

Abiria mwingine Happy Muhagama amesema yeye amelipa Sh 40,000 kwenda Iringa badala ya Sh28,000 ambayo ni bei elekezi.

"Wakati mwingine inabidi utoe fedha unayotajiwa iliuondoke, unakuta hakuna shida ya usafiri lakini kutokana na ongezeko la abiria wanasema hakuna usafiri au nafasi zimejaa lakini sio kweli unapotajiwa kiwango flani inabidi utoe tu," amesemaMuhagama.

Hata hivyo, msimamizi wa basi la Nazareti, Amina Salum amesema baadhi ya abiria wanampa fedha mtu yoyote badala ya kwenda ofisini ndio maana kumajitokeza changamoto hizo.

 "Ninachoona hapa ni elimu wakati mwingine sisi hatuji chochote lakini, abiria wanapaswa kupewa elimu namna ya kukata tiketi badala ya kumpa mtu yoyote," amesema Amina.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad