BUNDI analia Msimbazi.Mambo yanaonekana sio mazuri baada ya Mtendaji Mkuu, Barbara Gonzalez kuandika waraka wa kuachia kiti hicho cha moto.
Uvumi mwingi unazagaa kuhusu hatima ya mwekezaji. Mohammed ‘Mo’ Dewji huku timu imejikuta ikifanyiwa kebehi za kila aina kwenye mitandao ya kijamii na kwingineko baada ya kikosi cha Simba kuonekana kikiingia kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa kwa ajili ya mechi yao ya Kombe la ASFC kikitumia usafiri wa Toyota Coaster badala ya basi bao la kubwa la kifahari. Mambo ni mengi.
Sasa ngoja nikufahamishe kitu kuhusu huu uvumi uliousikia kwamba basi la wachezaji la Simba walilopewa na kampuni ya Africarriers linashikiliwa na wadhamini hao. Mwanaspoti limejiridhisha jambo hilo ni la kweli na sababu ni kwamba kuna mvutano wa kimkataba kwa pande zote mbili.
Wachezaji wa Simba na benchi la ufundi wanapokwenda uwanjani kwenye mazoezi Simba Mo Arena au Benjamin Mkapa wamekuwa wakitumia magari mawili aina ya Toyota Coaster, sababu gari lao limeshikiliwa.
Barbara aliyetoa notisi ya mwezi mmoja kuachia kiti chake cha Ofisa Mtendaji Mkuu, amekuwa haelewani kwenye masuala ya kimkataba na kampuni hiyo inayodaiwa kuwa chini ya baadhi ya viongozi wa Simba akiwemo, Fatema Dewji.
Ukiachana na ishu ya mivutano, kuna mambo mengine uongozi wa Simba hautakiwi kuyachukulia poa kwani ikishindwa kuyarekebisha kwa haraka mafanikio kwao itakuwa ndoto.
BODI KUVUNJIKA
Kama ulipata nafasi ya kuangalia au rudia tena kuangalia picha za mwisho zilizowekwa kwenye mitandao ya kijamii ya Simba ikionyesha Bodi wa Wakurugenzi ya klabu hiyo imekutana na kufanya kikao.
Utagundua kuna wajumbe wachache pengine kuliko vikao vingi vilivyowahi kufanyika huko nyuma ingawa kuna baadhi ya wajumbe walikuwa mbali na eneo hilo ambao walipata nafasi ya kuhudhuria kupitia mtandao.
Nguvu na uamuzi ya kikao hicho cha bodi si kama ilivyokuwa hapo awali, kwanza ilikuwa lazima wakutane wahusika wote na kila mmoja alikwenda kufanya kazi yake kulingana na majukumu aliyopewa kwenye kikao hicho.
Baadhi ya wajumbe hawana nguvu na moyo kama ilivyokuwa awali, ikielezwa mioyo yao imevunjika kutokana na baadhi ya mambo kwenda tofauti na matarajio yao huku kiongozi mmoja wa juu na mwenye nguvu (jina lake tunalo), alijiondoa hadi kwenye makundi ya WhatsApp kwa kushindwa kuwa na maelewano mazuri, ingawa jambo hilo baadaye lilisuluhishwa.
VIGOGO WAGAWANA
Kwenye misimu minne iliyopita, Simba ilikuwa moto kwenye mashindano ya ndani ikichukua ubingwa wa Ligi Kuu Bara awamu zote mfululizo pamoja na kufanya vizuri kwenye mashindano ya kimataifa (CAF).
Viongozi wa Simba inaelezwa wakati huu wamegawana kwenye kuongoza na kuendesha timu tofauti na hapo awali walikuwa wakikubaliana wote kwenye kila jambo ambalo walitakiwa kulifanya.
Ukiangalia vigogo wa juu Simba, Crescentius Magori amejiweka pembeni kwa kuomba kupumzika masuala yote ndani ya timu hiyo ikiwemo kusimamia usajili na si yeye pekee, bali kuna wengine watatu (majina yao tunao), wamejiweka mbali na timu.
Halikuwa jambo la kushangaza kuwaona, Zacharia Hanspoppe (marehemu kwa sasa), Mohammed Nassoro, Mulamu Ng’hambi, Barbara, Try Again, Magori na wengineo ukiwaona kwa pamoja kwenye matukio muhimu.
Viongozi hao kila mmoja alikuwa na majukumu yake kuhakikisha timu inafanya vizuri na walifanikiwa ila kuanzia msimu uliopita kutokana na kutokuwepo maelewano mazuri kati yao umoja huo uliondoka.
Kwa mfano msimu huu Simba inaweza kusafiri kwenda kwenye mechi za ugenini kiongozi akiwa ni mmoja tu, Ofisa Habari, Ahmed Ally, jambo ambalo ni tofauti na hapo awali.
USAJILI DIRISHA KUBWA
Kikao cha bodi kilichofanyika mara ya mwisho kilizuia mambo mengi ikiwemo usajili wa misimu hii miwili kwa maelezo kwamba haukuwa mzuri kutokana na zoezi hilo kusimamiwa na watu wachache na muda mwingine kuna wengine hawakushirikishwa.
Usajili wa madirisha mawili msimu uliopita, walisajiliwa kina Duncan Nyoni, Yusuph Mhilu, Abdulsamad Kassim uliibua maneno mengi kwani baadhi ya wajumbe wa bodi walieleza hao si daraja la wachezaji wa kucheza Simba.
Pia usajili wa dirisha kubwa msimu huu pia uliibua mengi, baadhi ya wajumbe wakiamini kuna makosa yaleyale ya msimu uliopita yamerudiwa tena.
Ulikuja mjadala mkubwa na mvutano wa aina yake hadi kufikiwa uamuzi kwamba usajili wa Simba kuanzia kwenye dirisha dogo lijalo Desemba 15 wanatakiwa kushirikishwa wote ili kila mmoja kutoa mawazo yake kwa wachezaji wapya na wale wa kuachwa.
Mvutano huo mkubwa uliibua maneno mengine makali na ulisababisha hadi baadhi ya vigogo kuamua kujiweka mbali na masuala hayo ya usajili tofauti na ilivyokuwa hapo awali.
NGUVU NDOGO YA MO DEWJI
Misimu minne Simba ikiwa kwenye kiwango bora, ilichukua mataji mbalimbali katika mashindano ya ndani na kufanya vizuri kimataifa (CAF) ikiweka rekodi mbalimbali. Kwa kiasi kikubwa nyuma yake kulikuwa na nguvu ya mdhamini, Mo Dewji wakati huo akiwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi.
Mo Dewji tangu alipokabidhi nafasi yake ya awali kwa Try Again hakuwa anatoa nguvu kubwa ya kumwaga mkwanja kwenye maeneo mbalimbali kama ilivyokuwa hapo awali na kuna sababu alizokuwa akieleza mwenyewe.
Kati ya masuala yanayochangia Mo Dewji kutokuwa na msukumo mkubwa wa kutoa pesa kama hapo awali ni kuchelewa kukamilika suala la mchakato wa mabadiliko huku akiamini mwenyewe ndiye anayelipigania.
Mo Dewji amekuwa akieleza kwenye nyakati mbalimbali Simba imekuwa ikijiendesha kwa hasara kutokana na kutoa mkwanja mrefu huku ikiingiza kidogo na jambo la mwisho kuna pesa nyingi zinatumika bila uangalifu.
TRY AGAIN TU
Simba wakati huu kwa kiasi kikubwa ipo chini ya Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi, Try Again anayepambana maeneo mengi mbalimbali kuhakikisha maisha ndani ya timu yanakwenda vizuri na kupata matokeo bora.
Try Again, kupitia vyanzo mbalimbali vya mapato ndani ya Simba na nyakati nyingine kwa nguvu yake mwenyewe huhakikisha wachezaji na waajiriwa wote wanapata mishahara na bonasi zao kwa wakati.
Kama unavyofahamu nguvu ya mtu mmoja ni tofauti na nguvu ya wengi kama ikitokea wakati huu Try Again amepata changamoto inaweza kuifanya Simba kushindwa kufanya vizuri kwani huku nyuma hakuna mtu mwingine anayepambana kwa nguvu kama ilivyo kwake.
KUONDOKA KWA BARBARA
Suala la Barbara kuacha kazi ndani ya Simba ingawa ametoa notisi ya mwezi mmoja si la kulichukulia poa.
Kati ya sababu kubwa ni kutokuwepo kwa maelewano mazuri na bosi wake Try Again, kwenye mambo tofauti ya msingi huku kila mmoja akiamini mwenzake anashindwa kufanya yale yaliyo muhimu.
Kwa mfano, Try Again, alikuwa akimpatia muongozo wa kazi Barbara alishindwa kufanya walivyokubaliana, kuna nyakati alijipa likizo na kuondoka ofisini wakati wa mechi ngumu au kipindi muhimu kama cha usajili.
Mazingira yaliyosababisha kuondoka kwa Barbara yasipoboreshwa, yatamkuta na ajaye.
BONASI NA MISHAHARA
Masuala yote hayo yanayotokea kuna nyakati yanakwenda kuathiri mambo muhimu kama kushindwa kulipa mishahara na bonasi kwa wakati.
Watzania vichwa vyao vimejaa ugoro, mwandishi kwa taaluma yake ni wachunguzi. Hawezi andika kitu ambacho hajakithibitisha lakini shabiki anadhani kuwa ameandika ili gazeti liuzwe. Pokeeni maandiko ili mchukue hatua kuinusuru simba vinginevyo hamuisaidii simba mpaka pale itakapoanguka kabisa ndiyo mtashtuka na mtakuwa mmeshachelewa.Zaidi
Jibu
NesphoryNgingo_03
1h
Simba wanaonekana kuwa wendawazimu Kulipa mishahara na bonanzi Kwa wakati zikiwa source yake ni wapi? Itafika wakati hiyo mishahara na bonanzi havitakuwepo maana mtoaji hayupo Mtayumba kwelikweliZaidi
J