Dar es Salaam. Mwanafunzi wa Shule ya Chalinze Modern Islamic Pre and Primary iliyopo mkoani Pwani, Iptisum Slim, aliyebadilishiwa namba ya mtihani wa darasa la saba amefaulu kwa wastani wa A.
Sakata la Iptisum lilianza kusikika Oktoba 14, baada ya kusambaa kwa video inayomuonyesha akiomba msaada kwa Serikali, akihofia kupoteza haki yake ya kusoma, baada ya kupewa namba 39 ya mwintu mwingine badala ya namba yake halali 40.
Kutokana na hilo, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda alitangaza kufanya uchunguzi, kuiifungia shule hiyo ya iliyopo mkoani Pwani kuwa kituo cha mtihani kwa muda usiojulikana.
Hata hivyo leo Alhamisi, Desemba 1, 2022 matokeo ya mtihani wa darasa la saba yaliyotolewa na Baraza la Mtihani Tanzania(NECTA) yameonyesha Iptisum amefaulu kwa wastani wa A, kwa kupata alama A katika masomo manne na B katika masomo mawili.
Masomo aliyopata A ni Kiswahili, English, Maarifa na Sayansi huku aliyopata B ni Hisabati na Uraia.
Akizungumza na Mwananchi muda mfupi baada ya matokeo hayo kutangazwa, Iptisum, amesema siri ya yeye kufaulu ni kusoma kwa bidii amefurahi na kuwashukuru wote waliomsaidia kupaza sauti.
Wakati kuhusu nini angependa kusoma akiingia sekondari, amesema ni masomo ya sayansi huku ndoto zake zikiwa kuja kuwa daktari.
Akizungumzana Mwananchi, mama wa mwanafunzi huyo, Atwiya Mohamed, amesema amefurahisha na matokeo hayo kwa kuwa hawakutegemea na mazingira magumu ambayo mtoto wao alipitia wakati anafanya mtihani huo wa Taifa.
“Kwa kweli nimefurahi sana matokeo ya mwanangu, kwani kwa changamoto alaizopitia wakati anafanya mtihani haikuwa rahisi kufikiria kwamba angepata alama hizo katika mtihani wake, namshukuru kila mmoja aliyepaza sauti kuhusiana na sakata lake la kubadilishiwa namba ya mtihani,” amesema Atwiya.