.
DAKTARI bingwa wa magonjwa ya wanawake nchini, Godfrey Chale amesema msanii Wema Sepetu hana sababu ya kuendelea kulilia mtoto.
“Nimesoma na kusikia kilio cha Wema kutamani kupata mtoto kwa muda mrefu; najiuliza sijui kwa nini hataki kufikia mwisho wa maumivu yake.
“Dunia ya leo imeendelea kisayansi na kitabibu, kwa mwanamke kukosa mtoto limekuwa tatizo dogo ambalo linaweza kumalizwa kirahisi.”
Dk. Chale amesema, Wema anatakiwa kuchukua hatua ya kuwa karibu na madaktari ili wamsaidie kuondokana na tatizo hilo.
Amesema; siku hizi kuna huduma ya upandikizaji mimba iitwayo IVF au kitaalam hufahamika kama In Vitro Fertilization ambayo inatolewa kwenye hospitali kubwa.
Akizungumza bungeni Jumanne Mei 11, 2021 wakati akiwasilisha bajeti kuhusu makadirio ya mapato na matumizi ya fedha kwa mwaka 2021/22 ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, aliyekuwa waziri wa wizara hiyo Dk Dorothy Gwajima alisema katika kipindi cha mwaka 2021/22 Hospitali ya Taifa Muhimbili itaanza kutoa huduma ya IVF.
“Wema aende Muhimbili akawaone wataalam, watamsaidia kuondoa tatizo lake na kumrejeshea furaha aliyoikosa kwa muda mrefu,” alisema Dk.Chale.
Tangu kuanza kutolewa kwa huduma ya IVF yamejitokeza matatizo mengi hasa katika mfumo wa uzazi wa wanaume.
Miongoni mwa changamoto hizo ni pamoja na kutokuwa kabisa na mbegu, kuwa nazo zenye ubora hafifu na zisizo na mbio, mbegu chache na zinazorudi kinyumenyume au kufanya tendo mara kwa mara na hivyo kuathiri uzalishaji mbegu bora.
Idara ya Huduma za Afya ya Uingereza (NHS) imethibitisha ubora wa IVF na kueleza uwepo wa hatua sita zinazozingatiwa katika kukamilisha zoezi hili.
Hatua ya KWANZA ni; kusimamsha mzunguko wa kawaida wa hedhi. Katika hatua hii mwanamke hupewa dawa kwa njia ya kunusa ama sindano kwa muda wa wiki mbili ili kuboresha ufanisi wa dawa za hatua inayofuata.
Hatua ya PILI ni kuboresha uzalishaji wa mayai, ya TATU kukagua maendeleo ya hatua mbili za awali.
Hatua ya NNE ni; kuvuna mayai kutoka kwenye mwili wa mwanamke, TANO ni kurutubisha yai jambo ambalo hufanyika kwenye maabara ambapo wataalamu huunganisha yai na mbegu za mwanaume.
SITA na mwisho ni kuhamisha kiini tete kutoka maabara mpaka mji wa mimba.
Baada ya mayai kuvunwa, mama mjamzito mtarajiwa hupewa homoni maalumu ya kuuandaa mji wa mimba kuweza kubeba kiini tete.
Utaalamu wa IVF uligunduliwa miongo minne iliyopita na wanasayansi watatu wabobezi wa magonjwa ya uzazi kutoka nchini Uingereza ambao ni Profesa Robert Edwards, Dk. Patrick Steptoe na Dk. Jean Purdy.
Hivi karibuni mchumba wa Wema, Whouz alilalama mimba na mpenzi wake kuchoropoka na kuapa kupambana hadi nyingine ipatikane.
Juhudi za kumpata Whouzu ili azungumzie utayari wa kumpeleka Wema kupata huduma ya IVF inayokadiriwa kuwa na gharama ya shilingi kati ya milioni mbili na kumi hazikuzaa matunda.