MAJERUHI Albert Mrema dereva aliyekuwa akiendesha gari T 597 BWU, aina ya Toyota Prado, ambayo lilisababisha vifo vya watu watatu, mama na watoto wake wawili, naye amefariki dunia usiku wa kuamkia leo Desemba 02,2022 majira ya saa nane usiku.
Mrema, alikuwa amelazwa Hospitali ya Mlongazila katika Chumba cha Uangalizi Maalum (ICU), tangu kutokea ajali hiyo Novemba 26, mwaka huu, eneo la Kibamba, mkoani Dar es Salaam, baada ya gari lao kupoteza mwelekeo na kutumbukia kwenye bonde.
Ajali hiyo ilisababisha vifo cha Immaculata Byemerwa (mama) na watoto wake, Janaeth Byemerwa aliyekuwa mwaka wa tatu, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), akisomea Uhandisi Ujenzi (Bsc.Civil Engineering) na Jollister Byemerwa, aliyehitimu kidato cha nne mwaka huu.
Kaka wa marehemu Immaculata, Patrick Mpocholwa ameiambia Nipashe Digital leo kuwa, majeruhi Albert naye amefariki dunia usiku wa kuamkia leo.
Familia hiyo ilipoteza maisha siku hiyo wakati ikitokea kwenye mahafali ya Jollister ya kidato cha nne katika Shule ya Sekondari Gili iliyopo Kibaha mkoani Pwani.