Dk Slaa aibuka kasoro kanuni za uchaguzi



Dar es Salaam. Aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Sweden, Dk Wilbroad Slaa ameibuka na kukosoa kanuni za uchaguzi zinazotumiwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuendesha chaguzi, akisema zimetungwa kinyume na Katiba ya nchi.

Kupitia mahojiano na Mwananchi kwa njia ya simu jana, Dk Slaa ambaye aliwahi kuwa Katibu Mkuu wa Chadema, alisema kuhusu kanuni hizo kama Katiba haijakaa vizuri Serikali ina uwezo wa kuziingilia muda wowote. “2015 watu wengi walienguliwa kutokana na kanuni zilizotengenezwa bila kufuata Katiba na sheria za nchi.

“Katika nchi yenye Katiba nzuri, kanuni haziwezi kutengenezwa na watu wakalazimishwa kusaini, huko nyuma tulilamishwa kuzisaini nikiwa mmoja wa waliolazimishwa kufanya hivyo, sasa hii haiko sawa kwa nchi inayofuata utaratibu wa kisheria,” alisema.

Akijibu hoja hiyo, Mkurugenzi wa Uchaguzi NEC, Dk Charles Mahera alisema vyama vya siasa husaini fomu za maadili ya uchaguzi na si kanuni.


“Kwenye uteuzi kuna mambo ya kuwekeana pingamizi, mfano mwaka 2020 kulikuwa na rufaa 165 za ubunge, kati ya hizo 98 walikuwa tayari wameenguliwa na 67 waliwekewa pingamizi ya kuenguliwa, kati ya wagombea 98 walioenguliwa NEC iliwarejesha 67 na 31 wakakosa sababu za msingi, hivyo tuliwaengua watu watatu kati ya 165 na 135 tukawarejesha,” alisema.

Dk Mahera alisema, kanuni haziwezi kuandaliwa bila kufuata sheria, hivyo hoja ya Dk Slaa haina msingi na kama wadau wanaona changamoto kwenye sheria wanajua nini cha kufanya.

Mwarobaini anaoutaja Dk Slaa wa kuondokana na changamoto hiyo ni Katiba mpya ambayo hutengeneza taasisi isiyoingiliwa na mamlaka yoyote.

“Unapoona Katiba ya nchi ni nzuri inatengeza taasisi ambayo haiwezi kuingiliwa na mamlaka, hatuna taasisi, kila kitu tunategemea mkuu wa nchi, mkoa au wilaya kwa hiyo tunategemea mapenzi ya watu badala ya taasisi za Taifa. “Rais Samia Suluhu Hassan anazunguka mataifa mbalimbali kuvuta wawekezaji, mazingira mazuri ya nchi yanaanza kuonekana kwenye Katiba, nchi ikiyumba kisiasa wawekezaji huogopa kuja.”

Alisema Taifa limepoteza fedha na muda kwenye suala la kikosi kazi ambao ungetumika kuandaa Katiba mpya. Hoja hiyo inaungwa mkono na mchambuzi wa masuala ya siasa, Greyson Mgonja aliyesema misingi haikuzingatia sheria kuanzisha kikosi kazi.

Kwa upande wa Makamu Mwenyekiti wa ACT wazalendo (Bara) Dorothy Semu alisema, wameunga mkono mawazo ya kikosi kazi kwani ni matokeo ya mikutano ya Baraza la Vyama vya Siasa.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad