Feisal Toto Mnyama Sana, Ainyima Prisons Mamilioni ya Pesa


YANGA inaondoka na pointi tatu kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara kwenye Uwanja wa nyumbani Benjamin Mkapa baada ya kuifunga Tanzania Prisons bao 1-0.


Bao la Yanga, lilifungwa dakika 89 na kiungo fundi, Feisal Salum baada ya mabeki wa Prisons kushindwa kuokoa shambulizi la nguvu kutoka kwa wapinzani wao.

Bao hilo kwa Feisal linakuwa la tano msimu huu akiwavukuzia vinara wa ufungaji, Fiston Mayele wa Yanga na Moses Phiri wa Simba wote wakiwa na mabao kumi.

Ushindi huu unakuwa na maana kubwa kwa Yanga kwenda kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Bara baada ya kufikisha pointi 35, katika michezo 14, iliyocheza msimu huu hadi sasa.


Kwenye mechi 14, za Yanga imeshinda 11, imetoka sare mbili, imefungwa moja, imefunga mabao 25, imefungwa mabao nane imefikisha pointi 35.

Wananchi baada ya mchezo huu imebakiwa na mchezo mmoja Jumatano itacheza dhidi na Namungo katika Uwanja wa Majaliwa Lindi ili kukamilisha mzunguko wa kwanza.

Kabla ya mchezo huu rekodi ya mechi tano nyuma inaonyesha Yanga ilishinda mechi nne na kufungwa moja iliyopita dhidi ya Ihefu kutokea Mbeya.

Tanzania Prisons baada ya kupoteza mchezo huu, inakwenda hadi nafasi ya 11, kwenye msimamo wa ligi ikiwa imecheza mechi 15 imeshinda tatu, imetoka sare sita, imefungwa sita, imefunga mabao 11, imefungwa mabao 15, imebaki na pointi 15.


Rekodi inaonyesha Prisons kabla ya kucheza na Yanga ilikuwa imefungwa michezo mitatu na kutoka sare mbili hivyo kutokana na matokeo ya leo imecheza michezo sita pasina kupata ushindi.

Feisal anakwenda kuweka rekodi ya kuwafunga, Prisons kwa mara ya pili mfululizo kwenye michezo ya Uwanja wa Benjamin Mkapa.


Baada ya mechi kumalizika, Feisal amesema mchezo ulikuwa mgumu kutokana na ubora wa wapinzani ila kikubwa timu imefanikiwa kupata ushindi.

“Muhimu ni pointi tatu kama timu tulikuwa tunazihitaji nashukuru Mungu bao langu limekwenda kukamilisha malengo haya,” amesema Feisal.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad