Treni ya Shirika la Reli Tanzania (TRC)
SHIRIKA la Reli Tanzania (TRC), limetoa nauli pendekezwa za abiria kwa treni ya njia ya Reli ya Kisasa (SGR), ambapo nauli ya mkubwa kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma Sh. 59,494 huku ya mtoto ikiwa ni Sh. 29,747, kwa daraja la kawaida. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam…(endelea).
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana tarehe 8 Desemba 2022 na Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano cha Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA), TRC imepanga nauli ya daraja la kati kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma, kuwa ni Sh. 71,392, huku ya mtoto ikiwa ni 35,696.
Taarifa ya LATRA inaonyesha kuwa, TRC imepanga nauli ya daraja la kawaida kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro kwa mkubwa Sh. 24,794, huku ya mtoto ikiwa ni 12,397. Wakati daraja la kati kwa umbali huo nauli ikiwa ni Sh. 29,752 kwa mkubwa na mtoto ni Sh. 14,876.
Hali kadhalika, taarifa ya LATRA inaonyesha nauli pendekezwa zilizotolewa na TRC kituo hadi kituo, ambapo ni wastani wa zaidi ya 4,000.