Dar es Salaam. Uamuzi wa Mahakama Kuu wa kubatilisha kuondolewa kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad katika nafasi yake umezua mjadala wa kikatiba.
Baadhi ya wanasheria wametoa maoni tofauti kuhusu hatima ya CAG Kichere baada ya hukumu hiyo wakisema kuna mengi ya kujifunza kutokana na uamuzi unaobainisha kulikuwana uvunjifu wa Katiba uliofanywa na Rais John Magufuli.
Juzi, jopo la majaji watatu, Dk Benhajj Masoud (kiongozi wa jopo), Juliana Masabo na Edwin Kakolaki walitoa uamuzi huo baada ya kesi ya kikatiba iliyofunguliwa na Kiongozi wa ACT Wazalendo, Zitto Kabwe.
Profesa Assad aliteuliwa kushika wadhifa huo kwa miaka mitano na Rais wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete kuanzia Novemba 5, 2014 na alihudumu katika nafasi hiyo kwa miaka mitano hadi Novemba 4, 2019 baada ya Rais wa awamu ya tano, Hayati John Magufuli kumteua Kichere kushika wadhifa huo.
Taarifa ya Ikulu ilieleza Rais alimteua Kichere baada ya Profesa Assad kustaafu na wakati huo (Novemba 2019), alikuwa amefikisha umri wa miaka 58, hivyo alikuwa amebakisha miaka miwili ya kustaafu ambayo ilitimia Oktoba 6, 2021 akiwa nje ya ofisi.
Wakizungumzia uhalali wa CAG Kichere, wanasheria hao walisema hapaswi kuendelea kuwa ofisini, huku wengine wakibainisha kuwa jambo hilo limepitwa na wakati na Mahakama ilitoa tamko lakini si kubatilisha uteuzi wa Kichere.
Wakili katika kesi hiyo, Dk Rugemeleza Nshala alisema uamuzi wa Mahakama wa kuondolewa kwa Profesa Assad ulikuwa kinyume cha Katiba, maana yake hata uwepo wa Kichere ni kinyume cha Katiba.
Alidai kuwa kutokana na uamuzi wa Mahakama ni kwamba, sasa kuna CAG wawili, Profesa Assad aliondolewa kinyume cha Katiba na Kichere naye akiwa bado ofisini kama mteule halali wa Rais.
“Profesa Assad aliondolewa kabla hajafikisha umri wa kustaafu wa miaka 65, na kwa kuwa hadi sasa hajafikisha umri huo, basi anastahili kurudi ofisini kwa mujibu wa tamko la Mahakama,” alisema Dk Nshala, aliyewahi kuwa Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS).
Dk Nshala alisema jambo la kujifunza kwenye hukumu hiyo ni kwamba watu wote ni sawa mbele ya sheria na kutokana na uamuzi huo, CAG watakaofuata watalindwa na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Wakili Dk Onesmo Kyauke alisema kama umri wa kustaafu wa Profesa Assad umepita basi jambo lake litakuwa limepitwa na wakati na Mahakama ilikuwa inatoa tamko tu kwenye shauri lililokuwa mbele yake.
Alitolea mfano kufukuzwa kwa wabunge wa Chama cha Wananchi (CUF) akisema Mahakama ilibainisha kufukuzwa kwao hakukuwa sahihi, lakini hawakuweza kurejea kwa sababu muda wa ubunge wao ulikuwa umekwisha.
“Kama huyo (Profesa Assad) alikuwa hajastaafu, Mahakama ingeweza kusema (Kichere) akae pembeni kwa sababu imejiridhisha kuwa huyu aliondolewa. Lakini kama muda wake ulishakwisha, hatuwezi kutengua uteuzi wa huyu kwa sababu aliteuliwa kihalali,” alisema Dk Kyauke.
Rais wa zamani wa TLS, John Seka hakutaka kuzungumzia uhalali wa CAG Kichere, akisema hukumu yenyewe imekwepa jambo hilo licha ya ombi kutolewa na upande wa mashitaka.
Seka alisema majaji walisema wamezingatia uhalisia Kichere alikabidhiwa madaraka na ameendelea kufanya kazi kwa mujibu wa Katiba, ameshafanya ukaguzi wa Serikali na ulipokelewa bungeni.
“Mlalamikaji amesema atakata rufaa na ametoa sababu ambazo ukiziangalia ni za msingi,” alisema wakili Seka.
Kuhusu mafao, Seka alisema, “hilo ni suala ambalo yeye (Profesa Assad) atadai kwa sababu yeye hakwenda kudai, bali aliondolewa kimakosa, aliyekwenda ni Zitto, kwa hiyo akitaka mafao yake atafuata mchakato unavyokuwa.”
Hata hivyo, gazeti hili kwa nyakati tofauti tulimtafuta Profesa Assad kwa njia ya simu lakini hakuweza kupatikana.
Mwanasheria mkongwe, Alute Mughwai Lissu alisema ili kuondokana na uvunjifu wa Katiba kama huo, wananchi wanatakiwa kupiga kelele hasa vyombo vya habari ili watawala wasiwe na nafasi ya kufanya wanachotaka.
“Tunahitaji kuwa na umma ulioamka na umma unaamshwa na vyombo vya habari vinavyofanya uchunguzi na kuuliza maswali magumu ili kupata majibu na wananchi wapate kuelewa,” alisema Alute.