MWANAMKE mrembo katika soka letu, Barbara Gonzalez ameachia nafasi yake. Anaweza kuwa mwanamke aliyekuwa na cheo kikubwa zaidi katika soka nchini. Mtendaji Mkuu wa klabu kubwa na kongwe nchini, Simba.
Kuachia kwake ngazi ni fumbo kwetu kuanza kusoma alama za nyakati. Kuna mambo mengi ndani yake. Sidhani kama imekuwa kitu cha kawaida. Kuna jambo fulani kubwa inawezekana linakuja pale Msimbazi kwa sasa.
Sioni kama mmiliki wa timu ataendelea kuwa klabuni hapo kwa muda mrefu. Yeye ndiye aliyetuletea mrembo wetu katika soka. Ni mtu aliyemuamini zaidi kusimamia maslahi yake klabuni hapo. Kabla ya Barbara kushika nafasi hii alikuwa msaidizi wake binafsi katika shughuli zake nyingine za kikazi na biashara.
Ni kitu cha kawaida kwa tajiri kulinda maslahi yake katika sehemu ambayo anaweka pesa zake. Nadhani ndio maana watu wa Simba walielewa uteuzi wa Barbara moja kwa moja licha ya kwamba alikuwa mgeni katika shughuli zetu za soka.
Siku chache kabla ya Barbara hajatuandikia barua ya kujiuzulu kulikuja uvumi kwamba tajiri anataka kuuza hisa zake pale Msimbazi. Kwa sasa tunaanza kuamini kwamba huenda uvumi ule ulikuwa na ukweli ndani yake. Labda umekuwa mpango madhubuti kwao kuondoka klabuni hapo.
Barbara amedai kwamba anaondoka pia kwa ajili ya kupisha bodi mpya ijayo ya timu hiyo kumchagua mtendaji wanayemtaka. Sidhani kama kikatiba analazimika kuondoka kwa ajili ya kupisha bodi mpya. Angeweza kuendelea kuitumikia bodi mpya chini ya tajiri huyu huyu aliyepo klabuni.
Tukiachana na hili la kwamba labda ni mpango wao na tajiri kuondoka klabuni hapo, lakini ukweli ni kwamba Barbara alikuwa anapigwa vita kubwa na wanaume waliomzunguka klabuni hapo katika shughuli za kila siku za kuiendesha Simba.
Wanaume waliamini kwamba Barbara alikuwa ni kiburi, mwenye nguvu na ambaye hakutaka kumsikiliza yeyote katika shughuli za uendeshaji wa Simba. Waliamini kwamba kwa sababu alikuwa ameletwa na tajiri basi alikuwa na nguvu kubwa kuliko kila mtu klabuni na alikuwa anachukua maamuzi yake binafsi.
Watu hawa hawa walikuwa wanaamini kwamba Barbara alikuwa anairudisha nyuma timu. Ilikuwa ni suala la muda tu kuona nguvu yake itaishia wapi. Alikuwa anapigana vita ngumu na watu ambao walikuwepo Simba kwa muda mrefu kabla yake.
Watu hawa hawa walikuwa wanataka ukongwe wao na uanaume wao viheshimiwe zaidi katika maamuzi ya kila siku klabuni. Vita hii ilimuacha Barbara akiwa na kundi dogo ndani ya klabu huku walio wengi wakiwa dhidi yake. Kilichoendelea kumuweka zaidi klabuni ni kwamba alikuwa amewekwa katika nafasi yake na tajiri wa timu.
Kama angekuwa ameingia klabuni kama walivyoingia watendaji wengine wa Simba na Yanga basi si ajabu angekuwa ameng’olewa mapema zaidi. Hata hivyo ilikuwa ngumu kuondolewa kwa sababu maslahi ya tajiri yalikuwa yanapitia kwake.
Hiki kilichoitwa kwamba Barbara alikuwa kiburi kinaweza kuwa na tafsiri tofauti katika soka letu. Ninachofahamu ni kwamba Barbara alikuwa amenyooka. Tatizo kubwa katika taasisi zetu ni watu kujaribu kuendesha mambo kwa mazoea. Ukipeleka mfumo tofauti wa utendaji kazi na kugusa maslahi ya watu ni rahisi tu kuonekana kwamba wewe ni kiburi.
Si ajabu hili ndilo ambalo lilimponza Barbara. Kwa nje Simba kulionekana kuko shwari lakini kwa muda mrefu tu Simba imekuwa ikipitia katika kipindi kigumu cha mabosi kupimana ubavu. Kuna nyakati ambazo naambiwa Barbara aliachiwa timu peke yake.
Tukiachana na hili, ni wakati wa kutafakari pia ukweli ambao umekuwa ukizizunguka Simba na Yanga kwa muda mrefu. Kwamba upande mmoja mambo yakiwa shwari basi upande mwingine mambo yanaanza kuharibika. Inadaiwa ndani na nje ya uwanja mambo yakiwa shwari upande mmoja basi upande mwingine kunaharibika.
Kule kwa wapinzani wao Yanga mambo hayakuwa shwari baada ya kuondoka kwa tajiri aliyepita, Yusuf Manji. Yanga wakapitia kipindi kigumu huku Simba wakitamba na tajiri wao kwa mafanikio ya ndani na nje ya uwanja.
Simba walitwaa ubingwa wa Ligi Kuu kwa miaka minne huku Yanga wakiwa na timu mbovu uwanjani lakini pia maisha magumu nje ya uwanja kiasi kwamba rafiki zangu, Mwinyi Zahera aliyekuwa kocha, pamoja na nahodha wake, Ibrahim Ajibu walikuwa wakichangisha michango hadi ya kusafirisha timu.
Sasa hivi kibao kinaelekea kugeuka. Yanga chini ya GSM wanaonekana kutamba ndani na nje ya uwanja. Wametengeneza timu nzuri uwanjani lakini nje wana maslahi mazuri. Simba kwa sasa tumeanza kusikia habari mbaya kutoka kwao. Mara wachezaji hawajalipwa bonasi zao, mara basi la timu limeshikiliwa na waliowapa.
Ndani ya uwanja pia ushindi umekuwa sio jambo la uhakika sana kwa Simba tofauti na ilivyo Yanga ambao walicheza mechi 49 za Ligi Kuu bila ya kupoteza na wapo katika nafasi nzuri ya kutetea ubingwa wao waliotwaa msimu uliopita.
Tumaini pekee la Wanasimba kwa sasa ambalo wanajinasibu kwa watani zao ni kufanikiwa kutinga katika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa wa Afrika. Hata hivyo, kuondoka kwa Barbara hakuonyeshi dalili njema ya kumalizika salama kwa msimu wao ndani na nje ya uwanja.
Kama kuondoka kwake kunahitimisha safari ya tajiri klabuni hapo, nani atasajili wachezaji katika dirisha la Januari linalosubiriwa kwa hamu na mashabiki wanaotaka kuona kikosi chao kinaimarishwa? Kwa sababu, sio siri hawawaelewi vema wachezaji kama Kibu Dennis na Pape Ousmane Sakho.