Jiji la Dodoma Lazika Maiti 59 zilizokosa Ndugu



Dodoma. Kutokana na maiti kukosa ndugu wa kuzipa heshima ya mwisho, Halmashauri ya Jiji la Dodoma imezika jumla ya maiti 59 zilizopokelewa katika kipindi cha Januari hadi Desemba 19.

Mapema mwezi huu, gazeti hili liliibua sintofahamu ya miili 19 iliyokuwa imekosa ndugu hivyo kutakiwa kuzikwa kwa mujibu wa sheria inayoelekeza mwili kukaa chumba cha kuhifadhia maiti kwa muda usiozidi siku 14.

Desemba 19, Halmashauri ya Jiji la Dodoma ilizika miili 12 kati ya 19 iliyokuwapo katika chumba cha kuhifadhia maiti cha Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma.

Akizungumza na Mwananchi jana, Ofisa Afya Usafishaji wa Jiji la Dodoma, John Lugendo alisema kuanzia Januari hadi Desemba 19 wamezika miili 59 ambayo marehemu waliokosa ndugu.

Katika kipindi hicho, Desemba ndiyo ulikuwa na maiti nyingi (12) na Januari zilikuwa chache zaidi, nne tu ingawa kuna miezi hawakuzika.

Miezi ambayo hawakuwa na miili ya kuzika ni Februari, Aprili, Julai na Septemba lakini Machi, Juni, Agosti na Novemba walizika miili saba huku OKtoba ikiwa minane.

Hata hivyo, Lugendo alisema katika miezi ambayo hawakuzika walibanwa na sheria.

Lugendo alisema maiti nyingi zinaozikwa na jiji ni za vijana ambao hufariki kwa ajali au wachache wanaugua.


“Baadhi tunazikuta na majeraha makubwa yanayohisiwa ni ya risasi au mapanga hasa vijana wenye kati ya miaka 25 hadi 35,” alisema Lugendo.

Ofisa huyo alisema miili mingine hukaa chumba cha kuhifadhia maiti kwa kukimbiwa na ndugu hasa jamii ya wafugaji ambao hawana utamaduni wa kuzika.


Sababu nyingine alisema ni ndugu kuiogopa miili ya wapendwa wao hasa wenye rekodi ya matukio ya uhalifu.

Mtunza makaburi ya eneo la Kilimo Kwanza yanayotumika kwa maziko hayo, Benard Ndalije alisema wastani wa kuzika miili hiyo huwa ni mara moja kila baada ya miezi miwili ingawa wakati mwingine huwa kila mwezi.

“Mara nyingi tunashindwa kutambua mwili huu ni wa jinsia ipi kwani wanakuwa wamekaa muda mrefu kwenye majokofu hivyo wanakuwa wamekakamaa na haturuhusiwa kuwafungua, sisi kazi yetu ni kuzika,” alisema.

Sakata la kuibuliwa kwa miili hiyo lilitokana na mwili uliookotwa ukiwa kwenye kiroba Desemba 5 jirani na Sekondari ya Jamhuri ambao ulikuwa miongoni mwa iliyozikwa Desemba 19.

Mwili huo ulikutwa ukiwa kwenye kiroba jirani na shule hiyo iliyopo katikati ya jiji, mita 30 kuna kituo cha Polisi cha Kata ya Majengo.

Mhudumu wa chumba cha kuhifadhia maiti cha hospitali hiyo, Beda Anthony alisema miili 19 katika chumba hicho haikuwa na ndugu hivyo utaratibu wao ni kuikabidhi kwa halamashuri jiji ambao ndiyo wanaizika.

By Ramadhan Hassan

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad