KAMA noma na iwe noma! Ndivyo utakavyoweza kusema ni baada ya uongozi wa Azam FC kuwaandikia barua Yanga ikiwaomba kukamilisha usajili wa mastaa wake Fiston Mayele na Yannick Bangala.
Hiyo ikiwa ni siku moja ipite tangu Yanga waiandikie barua Azam ikiwataka viungo wao tegemeo, James Akaminko na Kipre Jr waliojiunga na timu hiyo, katika msimu huu.
Yanga waliiandikia barua Azam kuwahitaji viungo hao, mara baada ya kiungo wao Feisal Salum ‘Fei Toto’ kuandika barua ya kuomba kusitisha mkataba wake wa miaka miwili unaotarajiwa kumalizika 2024.
Hii ni vita kali kwenye usajili huu mdogo ambapo matajiri wa Azam wakiongozwa na mmiliki wa timu, Yusuf Bakhresa huku Yanga wakiongozwa na bosi wao, Ghalib Said Mohamed ‘GSM’ wameonekana kutinishia misuli.
Taarifa za kuaminika kutoka ndani ya uongozi wa Azam zinasema kuwa wenyewe wamekubali kufanya biashara ya kuwaachia viungo wake hao kwa sharti la wao kuwauzia Mayele na Bangala.
Mtoa taarifa huyo mwenye ushawishi wa usajili Azam, ameliambia Championi Ijumaa kuwa wao wapo tayari kuanza mazungumzo muda wowote kuanzia jana Alhamisi.
Aliongeza kuwa upo uwezekano wa biashara hizo mbili kufanyika za Akaminko na Kipre Jr kwenda Yanga na Mayele, Bangala kutua Azam katika dirisha hili dogo la usajili.
“Mabosi wa Azam wamekubaliana kwa pamoja kufanya biashara ya kuwauza Akaminko na Kipre Jr baada ya kupokea barua kutoka Yanga ikiwaomba wachezaji hao.
“Hiyo imekuja ni baada ya kupata taarifa za sisi Azam kumalizana na Fei Toto kwa ajili ya kumsajili kwa kuwataka tukae nao meza moja kufanya biashara kutokana na kiungo huyo kusitisha mkataba Yanga.
“Kikubwa wanataka kulipiza kwa kuandika barua ya kutuomba kufanya mazungumzo kwa ajili ya kuwasajili wachezaji wetu Akaminko na Kipre Jr.
“Tumeipokea barua yao na kuwajibu kuwa tupo tayari kuwaachia wachezaji hao, na leo (jana Alhamisi) baada ya viongozi wa Kamati ya Usajili ya Azam kukutana kujadiliana masuala ya usajili tukaonaq na sisi kupeleka maombi ya kuwataka kufanya biashara ya kuwanunua Mayele na Bangala katika kukiimarisha kikosi chetu, hivyo tunasubiria majibu yao.”
Mtendaji Mkuu (C.E.O) wa Azam, Abdulkarim Amin ‘Popat’ alizungumzia hilo na kusema kuwa: ” Bodi yetu itakaa kujadili barua ya Yanga iliyoandikwa na C.E.O wa Yanga, Mtine (Andre) ikihitaji huduma za wachezaji wetu Kipre JR na Akaminko (James).
“Soka ni biashara baada ya mchezo wetu dhidi ya Mbeya City, ndani ya siku saba bodi itakutana kujadili, hivyo tutazungumza na benchi la ufundi na baada ya hapo tutaongea na wachezaji wenyewe kama Yanga watafikia kile tunachokihitaji tutafanya biashara.
“Uzuri ni tumewajibu barua hiyo waliyoandika Yanga, duniani hakuna mchezaji ambaye hauzwi, tukimaliza mechi yetu na Mbeya City tutakaa pamoja viongozi kujadili biashara hii. Timu yetu inajitosheleza sana. Hatuna mahitaji ya mchezaji yeyote mpya kwa sasa,” alisema Popat.
STORI NA WILBERT MOLANDI, CHMPIONI IJUMAA