Karim Benzema ametangaza kustaafu soka la kimataifa, siku moja baada ya Ufaransa kushindwa na Argentina katika fainali ya Kombe la Dunia 2022.
Benzema alikosa michuano hiyo nchini Qatar kutokana na jeraha la paja na hakuweza kuchezea Ufaransa tena.
Alicheza mechi 97 na anashika nafasi ya tano kwenye orodha ya wafungaji mabao wa muda wote wa Ufaransa akiwa na mabao 37.
"Nilifanya juhudi na makosa niliyochukua ili kuwa hapa nilipo na ninajivunia hilo!" Benzema alituma ujumbe huo katika mitandao yake ya kijamii. "Nimeandika hadithi yangu na yetu inaisha."
Mshambuliaji huyo wa Real Madrid na Ufaransa alishinda tuzo ya Ballon d'Or - tuzo ya mwanasoka bora wa mwaka huu - kwa mara ya kwanza.
Benzema alifunga mabao 44 katika michezo 46 alipoisaidia Real kushinda Ligi ya Mabingwa na La Liga msimu wa 2021-22.