Katumbi wa TP Mazembe ajitosa kuwania Urais DRC 2023


Mfanyabiashara maarufu, mwanasiasa na aliyekuwa gavana wa mkoa wa Katanga, Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo Moise Katumbi, ametangaza kwamba atagombea urais katika uchaguzi mkuu wa Desemba mwaka ujao 2023.



Katumbi, ambaye ni kiongozi wa chama cha Together for change yaani pamoja kwa ajili ya mabadiliko, alikuwa katika muungano mmoja wa kisiasa na rais wa sasa Felix Tshisekedi katika uchaguzi mkuu uliopita lakini anadai kwamba Tshisekedi ameshindwa kuiongoza nchi hiyo ya pili kwa ukubwa Afrika na yenye utajiri mkubwa wa madini.


Katika mahojiano na televisheni ya ufaransa, Katumbi amesema kwamba sababu yake kubwa ya kutaka kumuondoa Felix Tshisekedi madarakani katika uchaguzi mkuu wa mwaka ujao ni kutaka kusuluhsiha shida za Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo na kulijenga jeshi la nchi hiyo.


Katumbi amesema kwamba ukosefu wa usalama mashariki mwa Congo unatokana na jeshi lisilokuwa na uwezo wa kupambana na adui, na kwamba jeshi hilo limedharauliwa ndani na nje ya nchi kwa miaka mingi.


Umaarufu wa Katumbi DRC


Katumbi anajulikana kote nchini Congo kutokana na uongozi wake wa mkoa wa Katanga wenye utajiri mkubwa wa madini, pamoja na kumiliki timu ya soka ya TP Mazembe.


Lakini wachambuzi na wasomi wa siasa za DRC kama Marcel Saila akiwa Canada, anasema kwamba Katumbi, namna alivyokabiliwa na vizuizi kadhaa katika uchaguzi mkuu uliopita alipotangaza kugombea urais, ndivyo atakavyokabiliana na vizuizi vivyo hivyo kwa mara nyingine, hasa utata unaohusu uraia wake.


“Kuna watu DRC wanasema kwamba Katumbi sio raia wa Congo wa kweli kwa sababu babake ni mzaliwa wa Ugiriki na mama yake ni raia wa Zambia. Wakati akiwa gavana, alisemekana kuwa na pasipoti ya Italy. Alipata pasipoti ya Congo baada ya Tshisekedi kuwa rais. Kulingana na katiba ya DRC, ikishaomba na ukapewa uraia wanchi nyingine, unapoteza uraia wa Congo. Kwa hivyo hilo litakuwa tatizo kubwa kwake.”

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad