KUMEKUCHA...! Saido Apewa Masharti Magumu Kumwaga Wino Simba



SIKU chache kabla ya kufunguliwa kwa dirisha dogo la usajili, mabosi wa Simba wameonyesha kiu yao ya kumnasa kiungo fundi wa zamani wa Yanga, Saido Ntibazonkiza na habari za ndani zinasema jamaa amepewa masharti magumu naye ameweka yake mezani ili kama vipi amwage saini.

Mbali na Saido inaelezwa Simba inamezea pia kiungo mkabaji, Kelvin Nashon ‘Dudumizi’ anayekipiga Geita Gold.

Kwa dili la Saido, taarifa zinasema pande zote mbili zimewekeana masharti magumu na kila mmoja anatakiwa kukubaliana na mwenzake ili mkataba wa miaka miwili usainiwe fasta kabla ya kuanza kuwatumikia mabingwa hao mara 22 wa Ligi Kuu.

Saido alikuwa wa kwanza kuweka masharti amewaambia Simba ili akubali kusaini hatakuwa mchezaji anayekaa kambini timu inapokuwa jijini Dar es Salaam, bali atakuwa mchezaji wa kwenda mazoezini Mo Simba Arena na kwenye mechi kisha kurejea nyumbani kwake.


Hakuishia hapo staa huyo wa kimataifa wa Burundi, amewaeleza Simba anahitaji nyumba nzuri ya kuvutia ili aweze kuishi hapo na anataka iwepo maeneo matatu hapa Dar, Masaki, Mikocheni na Oysterbay tofauti na maeneo hayo hatakubaliana nao.

Baada ya hapo amewaeleza Simba yupo tayari kusaini mkataba wa miaka miwili, mshahara kwa mwezi anataka kuvuta USD 3,500 zaidi ya Sh7 milioni na pesa ya usajili USD 25,000 (zaidi ya Sh50 milioni) na anaitaka zote zitoke kwa pamoja.

Baada ya Saido kutoa masharti yake mabosi wa Simba walikubali kumpa nyumba na maeneo aliyochagua, mshahara wa kila mwezi na pesa ya usajili anaohitaji ila hawakukubaliana naye na suala la kutokukaa kambini pamoja na wachezaji wenzake.


Mabosi wa Simba walimweleza Saido anatakiwa kukaa kambini kama ratiba inavyotaka, suala la kuishi kwake wakati wenzake wakiwa kambini hawakubaliani nalo kwani litaleta mpasuko ndani ya timu na litavunja umoja.

Wakati mabosi wa Simba wakipinga suala hilo la kutokukaa kambini walimweleza wanamuwekea masharti anatakiwa kufuata taratibu zote za timu ndani ya uwanja, kambini na hata nje ya maisha ya uwanjani.

Saido anatakiwa kufuata masuala yote ya kinidhamu kama ilivyo kwa wachezaji wengine ikitokea amekwenda tofauti na makubaliano kwa maana ya kuvunja sheria na kufanya vitendo vya utovu wa kinidhamu kuna kiasi cha pesa atakuwa anakatwa ndani ya mkataba wake.

Wakati Saido akivutana na Simba kama watakubaliana atasaini mkataba kutokana na vipengine hivyo na kama wakishindwana dili hilo litakufa.Kama dili hilo litakwenda vizuri kazi itabaki kwa Simba kwenda kumalizana na Geita Gold kwani Saido alisaini mkataba wa mwaka mmoja na ameutumikia miezi sita na imebaki miezi sita.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad