MAAJABU! Mipira ya Kombe la Dunia Qatar inachajiwa kama simu




DOHA, QATAR. TEMBEA uyaone. Ushawahi kufikiria juu ya mpira wa soka wa kuchajiwa kama simu? Basi kama unafuatilia fainali za Kombe la Dunia 2022 za huko Qatar, mipira inayotumika huko yote inachajiwa kwa umeme kama simu tu.

Mipira inayotumika kwenye fainali za Kombe la Dunia 2022 imetengenezwa kwa teknolojia kubwa sana, ikiwekewa ‘chip’ maalumu ndani, ambazo zinahitaji kuwa na nishati ya umeme kufanya kazi kwa usahihi.

Picha iliyotumwa kwenye mitandao ya kijamii ikionyesha mipira ya soka inayotumika huko Qatar ikiwa inachajiwa, imewaacha kwenye mshangao mkubwa mashabiki huku wengine wakidai kweli duniani kuna mambo.

Mipira ya Kombe la Dunia 2022 iliyotengenezwa na Adidas ina sensa ndani yake, ambayo inakusanya takwimu mbalimbali, kasi na uelekeo wa mpira na kutuma ujumbe kwenye mashine za VAR kutambua kama kuna mchezaji ameotea (offside) au la.


Picha iliyowekwa kwenye mtandao wa Reddit inaonyesha mipira ikichajiwa kama simu za mkononi, ambazo zilichomekwa kwenye umeme kabla ya mechi za Kombe la Dunia 2022 huko Qatar, ambapo kwa sasa zinakamilisha hatua ya makundi.

Shabiki mmoja aliandika: “Hivi unahitaji app kufanya kazi?”

Mwingine aliongeza: “Kichwa cha habari za siku za baadaye: Mipira haikuchajiwa, mechi ya ubingwa imeahirishwa.”


Shabiki wa tatu aliandika: “Nazeeka sasa, nakumbuka kipindi kile tulichokuwa tukijaza upepo mipira.”

Sensa iliyopo ndani ya mpira huo, inapewa nguvu na betri ndogo, ambayo uwezo wake wa kukaa na chaji wakati ukitumika ni saa sita na chaji itadumu kwa siku 18 kama hautakuwa unatumika.

Uzito wa sensa hiyo ni gramu 14 ambayo kazi yake ni kufanya uelekeo wa mpira huku ikiwa imeunganishwa na kamera mbalimbali zilizopo uwanjani ili kuwasaidia waamuzi juu ya mchezaji kuotea na mambo mengine.

Maximillian Schmidt, mwanzilishi na mkurugenzi mtendaji wa KINEXON, ambao wametengeneza sensa hiyo amefunguka jinsi inavyofanya kazi ndani ya uwanja wakati mchezo ukiwa unaendelea. Mpira huo wa Kombe la Dunia 2022 unaitwa Al Rihla.


Schmidt alisema: “Muda wowote mpira utakapopigwa kwa mguu, kichwa, kurushwa hata ukiguswa tu, meseji 500 zinakuwa zimetumwa ndani ya sekunde.

“Data zimetumwa kwa wakati na haraka, kupitia antena za mtandao zilizowekwa kuzunguka uwanja wa mchezo na hivyo kuhifadhiwa kwenye kompyuta kwa ajili ya matumizi inapohitajika.

“Kama mpira utatoka nje ya eneo na kuingizwa mpira mwingine uwanjani, mfumo unakamata haraka na data zinanaswa zenyewe bila ya kuhitaji usaidizi wa kibinadamu.”

Adidas imetengeneza mpira mwepesi na wenye kasi kubwa, kitu ambacho kimemfanya beki wa England, Kieran Trippier kufichua umekuwa ukimpa shida kwenye kupiga mipira ya friikiki.


Trippier alisema: “Kila nilipojaribu kupiga mpira wakati wa adhabu ndogo niligundua kuna utofauti, lakini hicho hakiwezi kuwa kisingizio katika jambo lolote. Ninachoweza kusema ni kwamba mipira iko tofauti, sio ishu ya joto wala kingine. Nadhani mipira ni myepesi sana. Ukitumikia nguvu nyingi kupiga, unapaa.”
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad