Mahakama Yaamuru Mwili wa Marehemu Ufukuliwe, Uchunguzwe



Mwili wa mwanamke aliyefia mahabusu katika kituo cha Polisi Mburahati, Stella Moses sasa utafukuliwa ili ufanyiwe uchunguzi kubaini chanzo cha kifo chake, Mahakama ya Hakimu Mkazi Kivukoni (Kinondoni) imeamuru.

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kivukoni (Kinondoni) Dar es Salaam imeamuru kufanyika kwa uchunguzi wa chanzo cha kifo cha Stella Moses aliyefia mahabusu katika kituo Cha Polisi Mburahati mwaka 2020,


Uamuzi huo umetolewa leo Desemba 19, 202 na Hakimu Mkazi Mkuu, Franco Kiswaga, baada ya kukubaliana na maombi ya wanafamilia katika shauri la maombi walilolifungua mahakamani hapo.


Stella alifariki dunia usiku wa Desemba 20, 2020, akiwa mahabusu kituoni hapo alikojisalimisha baada ya kupata taarifa kuwa alikuwa anahitajika, tukio ambao lilizua mvutano mkubwa baina ya Polisi na ndugu wa marehemu kwa kile walichodai kuwa ni mazingira tata ya kifo hicho.


ALSO READ

Ujue utamu wa likizo Desemba

Kitaifa 15 hours ago

Serikali ya Kenya yapinduliwa Agosti-6

Kimataifa 15 hours ago

Polisi walidai kuwa alijinyonga, maelezo ambayo wanafamilia hawakukubaliana nayo badala yake wakaomba ufanyike uchunguzi huru kujiridhisha na chanzo cha kifo chake, lakini Jeshi la Polisi halikuwa tayari na badala yake lilishinikiza mwili wa marehemu uzikwe.


Hivyo mapema mwaka huu ndugu wa marehemu walifungua shauri la maombi dhidi ya viongozi wa Jeshi la Polisi na uongozi wa hospitali ya Muhimbili kwa kutokutimiza wajibu wao.


Shauri hilo lilifunguliwa na shemeji wa marehemu, Emmanuel Ernest Kagongo, kwa niaba ya familia ya marehemu dhidi ya dhidi ya Jeshi la Polisi akiwakilishwa na wakili Peter Madeleka.


Katika hati ya maombi hayo ya jinai mchanganyiko namba 3 ya mwaka 2022, aliomba mahakama hiyo iridhie kufanya uchunguzi huru ili kujua ukweli wa mazingira ya kifo cha ndugu yao.


Wajibu maombi katika shauri hilo ni Mkuu wa Jeshi la Polisi (Inspekta Jenerali wa Polisi – IGP), Kamanda wa Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam (ZPC) na  Kamanda wa Polis Mkoa wa Kipolisi Kinondoni (RPC).


Wengine ni Mkuu wa Polisi Wilaya ya Kipolisi Mburahati (OCD), Mkurugenzi Mkuu wa Hospitali ya Taifa Muhimbili na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.


Akitoa uamuzi wake baada ya kusikiliza hoja za upande mmoja wa mwombaji kutokana na wajibu maombi kushindwa kuwasilisha hoja zao za maandishi, Hakimu Kiswaga amesema kuwa anakubaliana na maombi hayo.


Hakimu Kiswaga amesema kwamba kutokana na hoja za mwombaji na viapo kinzani vya wajibu maombi watu waliowasilisha viapo kinzani kati ya sita hakuna ubishi kuwa Stella alifariki dunia katika mazingira tata akiwa katika kituo Cha Polisi Mburahati.


Amesema kuwa kwa kuwa wajibu maombi hususan Polisi hawakutekeleza wajibu wao wa kisheria yaani kutoa taarifa na hakuna taarifa zozote za uchunguzi uliofanyika kuonesha chanzo cha kifo hicho, zilizowasilishwa mahakamani basi mahakama hiyo ina jukumu la kuamuru ufanyike uchunguzi huo.


"Hivyo mahakama hii inaamuru ufanyike uchunguzi wa kifo cha Stella Moses ambaye mahakama hii inaona kwamba alifariki unnatural death (kifo kisicho cha kawaida) akiwa chini ya Jeshi la Polisi Mburahati, Desemba 20, 2020," amesema Hakimu Kiswaga na kuongeza:


"Taarifa (ya uchunguzi) itolewe mahakamani na ipelekwe kwenye vyombo husika ili aliyehusika na kifo hicho achukuliwe hatua za kisheria."

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad