Dodoma. Wauguzi wa Hospitali ya Taifa ya Afya ya Akili, Mirembe wameeleza namna wanavyopigwa na wagonjwa wa akili wakati wakiwahudumia, ikiwemo kujeruhiwa na kutemewa mate.
Takwimu za matukio ya namna hiyo zilizotolewa na hospitali hiyo zinaonyesha kuwa wauguzi watano walipigwa, mmoja alivunjwa mkono, mwingine alipasuliwa jicho na wawili walivunjwa mbavu.
Changamoto nyingine wanazokutana nazo wauguzi hao ni kutukanwa na kushikwa sehemu nyeti hususani wanawake, na kusababisha baadhi yao kuhama vituo vya kazi kutokana na kero hizo.
Akizungumza na Mwananchi kwenye mahojiano maalumu, Mkurugenzi wa huduma za uuguzi kutoka hospitalini hapo, Clavery Lyela alisema kuwa nguvu kazi zaidi ya miundombinu na rasilimali watu inahitajika kunusuru maisha ya wauguzi wa hospitali hiyo. Alisema hivi karibuni kumetokea matukio ya wauguzi watano kupigwa na kusababishiwa majeraha sehemu mbalimbali za miili yao.
“Kuna muuguzi alipigwa akavunjwa mkono, mwingine alipasuliwa jicho na wengine wawili walivunjwa mbavu, hii inatokana na taratibu zetu za uuguzi.
“Unaletewa mgonjwa ana pingu mkononi, lakini kutokana na taaluma yetu inabidi umfungue umtibu akiwa hana pingu ili ajione yuko huru na sehemu salama,” alisema.
Kwa mujibu wa Clavery, maisha ya wauguzi hao yapo kwenye hatari kwa kuwa hupokea wagonjwa wa aina tofauti, ikiwamo majambazi, wanajeshi, wafungwa na waraibu wa dawa za kulevya.
Clavery alisema muuguzi anatakiwa kumtoa mgonjwa kwenye mazingira ya kujiona mfungwa na kumuamini ili amhudumie.
“Kwa mamlaka za wenzetu kama polisi au magereza wanatumia pingu na bunduki, lakini sisi hatuna silaha wala mafunzo.
“Mgonjwa analetwa kashikwa na ndugu zaidi ya watano, lakini wewe unayemhudumia uko peke yako, hebu fikiria ni ngumu kiasi gani kwetu,” alihoji.
Alisema changamoto hizo zinahatarisha maisha ya wauguzi wa hospitali hiyo na kupunguza ufanisi wa kazi, kutokana na kujilinda ili kuepuka madhara.
Hata hivyo, alisema mikasa kutoka kwa wagonjwa sio changamoto pekee wanayokumbana nayo, bali hata mazingira ya kazi katika hospitali hiyo.
Alisema uhaba wa wauguzi unachangia kupata madhara, kwani matukio mengine hutokea wakati muuguzi yupo peke yake hana mwenzake wa kumsaidia.
Alisema hospitali hiyo ikijumuishwa na kitengo cha magonjwa ya afya ya akili Itega na Isanga ina jumla ya wauguzi 115, ikiwa na upungufu wa wauguzi 308 kufikia idadi ya wauguzi 423 wanaohitajika.
“Tupo wachache sana, sisi ni binadamu na wakati mwingine kuna kuumwa, kufiwa, kuuguliwa au kuwa likizo za uzazi, kwa hiyo upungufu unakuwa mara mbili yake,” aliongeza.
Clavery alisema kwa taratibu muuguzi anatakiwa afanye kazi saa nane, yaani atakayeingia saa 1:30 asubuhi atatoka saa 7:30, na nusu saa ya kukabidhiana mafaili hivyo kutimia saa 8:00 mchana.
Alisema muuguzi huyo atafanya kazi hadi saa 12:30 jioni na kumuachia anayetakiwa kufanya kazi zamu ya usiku.
“Kutokana na upungufu uliopo muuguzi analazimika kufanya kazi siku nzima, yaani asubuhi hadi usiku na wengine kukosa mapumziko siku za mwisho wa juma,” alisema.
Alisema upungufu huo pia huwafanya kukiuka kanuni za Shirika la Afya Duniani (WHO), zinazoelekeza mgonjwa mmoja hatarishi (anayedhuru), anapaswa kuhudumiwa na muuguzi mmoja.
Pia, alisema muuguzi mmoja anapaswa kuhudumia wagonjwa wa kawaida wanne hadi sita (wasiodhuru), wakati wa mchana na wagonjwa saba wakati wa usiku, jambo ambalo kwao haliwezekani. Aliongeza kuwa katika hospitali hiyo kuna wodi namba tatu na 13 ambazo huwahifadhi wagonjwa hatarishi. Alifafanua wodi 13 ina vyumba 18 kwa ajili ya wanaume na wodi tatu ina vyumba vinne kwa ajili ya wanawake.
Pia, alisema wodi za kawaida kwa wastani zina vitanda 24, lakini wagonjwa huzidi 30 hadi 40 na kukiwa na wauguzi wanane hadi tisa tu kwa zamu zote tatu.
“Kuna changamoto ya kuzidi wagonjwa, kama leo (jana) Isanga ambayo ina uwezo wa kuchukua wagonjwa 175 (wa mauaji) kuna wagonjwa 254 na kwa kanuni palitakiwa kuwe na wauguzi 42, tukiwapa kila mmoja wagonjwa sita, lakini hilo haliwezekani,” alisema.
Aliongeza kuwa wodi hizo za kawaida ambazo zina wagonjwa 30 hadi 40 zinalazimika kuwa na wauguzi wawili, ili kupokezana na kutimiza zamu zote tatu.
Clavery alisema changamoto hizo hutofautiana na changamoto za wauguzi wa hospitali nyingine, kutokana na mazingira ya kazi zao kuwa hatarishi na aina ya wagonjwa wanaowahudumia.
“Nitoe wito kwa wasomi kuingia zaidi kwenye sekta hii ili kuendelea kutoa huduma bora na Serikali iongeze nguvu kwa kuajiri wataalamu zaidi watakaoongeza nguvu kazi kwenye hospitali yetu, na kutuboreshea mazingira rafiki ya kazi zetu,” alisema.
Kauli ya wauguzi
Paul Mhina ni mmoja wa wauguzi waliopata madhara kutokana na kupigwa na mgonjwa, akiwa kwenye majukumu yake ya kila siku ya kutembelea wodi ya wanaume.
Paul alisema akiwa kwenye wodi ya wanaume muuguzi aliyepo zamu siku hiyo alimwambia kuna mgonjwa yupo kwenye hali hatarishi.
“Mgonjwa mmoja baada ya kusikia kauli ile akakimbia kwenda kumdaka yule nesi akitaka kumshambulia, ikabidi nisogee kuzuia, ndipo yule mgonjwa akanigeukia. “Nikajikuta nimepigwa ngumi kama nne au tano hivi usoni, ambazo zilinifanya nichanike mdomo, kupasuka sehemu ya jicho na jino moja kuning’inia,” alisema.
Paul ambaye amefanya kazi hospitalini hapo kwa miaka 30 alisema Serikali iangalie namna ya kuwapa wauguzi wa hospitali ya Mirembe posho za ziada za majanga ya kudhuriwa na wagonjwa wanaowahudumia.