MASTORI YA OSCAR: Miquissone ametuonyesha uhalisia wetu, Wabeba Mitumba



WACHEZAJI wa kigeni nchini huwa hawaachwi moja kwa moja. Usishangae siku Saido Ntibazonkiza akirudi tena Yanga. Usishangae Bernard Morrison akirudi tena Simba siku moja. Mzunguko mdogo wa wachezaji na viongozi ndio chanzo cha haya. Umewahi kujiuliza kwa nini Real Madrid wanalitawala soka la Ulaya muda mrefu sasa? Na pia kuwaacha wengine mbali sana kwenye mataji ya UEFA?

Haya ya Real Madrid yameletwa na uwepo wa fedha chini ya rais wa klabu hiyo, Florentino Perez pamoja na ushawishi wake. Kutokana na ushawishi wa huyu mzee ndio maana unaona wachezaji wengi wazuri wanatamani kucheza Real Madrid.
Angalia pale Manchester United wana pesa ila wanakosa ushawishi wa mtu kama Perez. Ndiyo maana usajili wao bado haujawalipa tangu kuondoka kwa Sir Alex Ferguson.

Wakati mwingine unaweza ukasema pesa haiwezi kukupa kila kitu, ila hiyo pesa kwa asilimia kubwa ndiyo itakupa kile ambacho unakitamani. Ukirudi hapa Afrika katika michuano ya Ligi ya Mabingwa utaona klabu za Ukanda wa Afrika Kaskazini ndizo watawala wa mashindano hayo.
Waangalie Al Ahly ya Misri, hawa jamaa wamechukua mara 10 Ligi ya Mabingwa Afrika. Unajua sababu ni nini? Jibu ni uwekezaji ambao unahitaji pesa.

TP Mazembe kuna wakati nao walikuwa na matumizi makubwa ya pesa ndio maana unawaona hadi sasa wameshinda mataji matano ya Ligi ya Mabingwa Afrika. Soka limekuwa ni biashara kubwa ndio maana unaona hapa kwetu tumekuwa tukisajili wachezaji wa kigeni, ila wale wengi wamemaliza mikatabao au wameachwa walikotoka.

Kila mwana Simba ukikutana nae kijiweni muulize, unataka Luis Miquissone arejee katika timu yako? Atakwambia ndiyo! Ila kwa sasa Miquissone amepanda thamani sio yule ambaye aliondoka Simba mwaka jana.

Hii inaonyesha kuwa bado klabu hasa hizi kongwe za Simba na Yanga hazina msuli wa kusajili mchezaji wa kigeni ambaye yupo ndani ya mkataba. Miquissone ametuonyesha uhalisia wetu.

Kwa sasa Miquissone ana mkataba wa miaka mitatu na mshahara wake ni zaidi ya Sh110 milioni. Je hawa Simba ambao wanahusishwa kumrejesha wako tayari kulipa hiyo fedha? Jibu unalo kichwani.

Inaweza ikatokea nchini klabu moja ikashinda taji la michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa sababu tu mpira wakati mwingine una matokeo ya kikatili, ila hilo jambo haliwezi kuwa na mwendelezo kama hakutakuwa na wachezaji wenye ubora mkubwa ambao wanapatikana kwa fedha nyingi.

Leicester City waliwahi kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu England (EPL) msimu wa 2015/2016 ila kwa sasa unawaona wanachopitia pale England. Ni wachovu tu. Ni watu wanaowaza kukwepa kushuka daraja kila msimu.
Ili Simba na Yanga zishindane na miamba mikubwa Afrika katika soka ni lazima ziwe na pesa ya kutosha ambayo itazisaidia kusajili wachezaji wenye thamani kama hawa kina Miquissone.

Twendeni taratibu huko mbeleni tunaweza kufika nchi ya ahadi katika soka la Afrika kwa upande wa klabu. Ukitazama makundi ya michuano ya klabu Afrika utagundua kuwa timu zetu zimepangwa na timu ambazo kimsingi hazitishi kabisa, lakini bado hatuna uhakika wa kufuzu.

Simba miaka mitano iliyopita walikuwa na kikosi cha maangalizi lakini hakipo kwa sasa. Yanga wameanza kujenga timu. Wamekuwa bora soka la ndani, lakini kimataifa bado ni wapiga ramli. Hakuna uhakika. Wanasuasua tu.

Ndiyo maana basi tunasajili wachezaji mtumba. Ndiyo maana basi tunasajili wachezaji wengi wenye umri mkubwa. Uzuri wa ligi yetu ya ndani ina maajabu kidogo. Wachezaji wakubwa ndiyo mastaa wa timu zetu.
Ni mara chache sana kuona mchezaji mwenye umri mdogo anakuwa supastaa Bongo. Mchezaji mwenye miaka zaidi ya 30 ni rahisi tu kuwa mchezaji bora wa ligi mwishoni mwa msimu. Mchezaji mwenye miaka 30 ni rahisi tu kuwa mfungaji bora. Linapokuja suala la kimataifa, timu zetu ni vibonde. Linapokuja suala la michuano ya kimataifa timu zetu ni mchekea. Bado usajili wetu ni wa kutambiana tu sisi kwa sisi.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad