Mayele Aiweka Yanga Pabaya leo Jumapili dhidi ya Tanzania Prisons kwa Mkapa



KOCHA Msaidizi wa Yanga, Cedric Kaze, ameweka wazi kuwa, kuna hatihati ya kuwakosa wachezaji wake muhimu katika mchezo wa leo Jumapili dhidi ya Tanzania Prisons kutokana na sababu mbalimbali akiwemo, Fiston Mayele.

Mayele ambaye ni kinara wa mabao katika Ligi Kuu Bara msimu huu akifunga kumi, amekuwa mchezaji tegemeo ndani ya Yanga na kukosekana kwake ni kuiweka pabaya timu hiyo kwenye mipango ya kutetea taji lao la ligi hiyo.

Yanga ambao leo watakuwa wenyeji wa Tanzania Prisons katika mchezo wa Ligi Kuu Bara utakaochezwa Uwanja wa Mkapa, Dar, pia inatarajia kumkosa Jesus Moloko na Dickson Job mwenye kadi tatu za njano.

Akizungumza na Spoti Xtra, Kaze alisema Mayele na Moloko hawakufanya mazoezi na wenzao juzi, hivyo suala la kucheza leo ni asilimia ndogo sana kutokana na kutokuwa fiti.


“Kuna wachezaji hawapo fiti kwa ajili ya mchezo dhidi ya Tanzania Prisons, mchezaji kama Fiston Mayele na Moloko wote hawakufanya mazoezi yaliyopita kutokana na kuwa majeruhi, tutaangalia kama wataweza kufanya mazoezi leo (jana Jumamosi) ili tuone kama tutawatumia. “Dickson Job pia hatatumika katika mchezo huu, huku Djuma Shabani, Farid Mussa wakiwa wamerejea ndani ya timu.

Morrison (Bernard) amerejea, lakini bado tunaangalia kama tunaweza kumtumia, Mwamnyeto (Bakari) na yeye hivyohivyo, naamini tutakuwa na mchezo mgumu lakini ni muhimu zaidi tukapata matokeo mazuri dhidi ya Tanzania Prisons,” alisema Kaze.

Kwa upande wa Nahodha wa Tanzania Prisons, Benjamin Asukile, alisema: “ Tumekuja kwa ajili ya kuhakikisha tunapata matokeo mazuri mbele ya Yanga, tupo tayari kwa mchezo na tutapambania haswa timu yetu ili tupate matokeo mazuri.” Rekodi zinaonesha kwamba, tangu msimu wa 2012/2013 timu hizi zilipoanza kukutana kwenye Ligi Kuu Bara mara 20, Yanga imeshinda mechi 11, Tanzania Prisons imeshinda 1, huku sare zikiwa 8. Uwanja wa nyumbani pekee, Yanga imecheza mechi kumi dhidi ya Prisons, kati ya hizo, imeshinda 6, sare 4, haijapoteza.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad