Dar es Salaam. Mwenyekiti wa chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania-Chadema, Freeman Mbowe ameeleza namna alivyokamatwa na viongozi wenzake Oktoba 30 mwaka 2020 na sababu za wao kukimbilia nje ya nchi.
Mbowe ambaye ni mbunge wa zamani wa Hai mkoani Kilimanjaro ameeleza hayo usiku wa kuamkia leo Jumapili Desemba 11, 2022 wakati akizungumza na wanadaispora wanaoishi Marekani.
Mwenyekiti huyo ambaye yupo Marekani ziarani kwa siku sita, ikiwemo kuhudhuria mkutano wa Umoja wa Vyama vya Demokrasia Afrika (DUA), akiwa yeye ni mwenyekiti mwenza wa umoja huo, amewaambia wanadaispora alikamatwa baada ya kumaliza kikao na viongozi wenzake wa upinzani.
Katika mkutano na wanadaispora Mbowe aliwaeleza Watanzania hao namna Taifa lilivyopitia baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 na misukosuko walioipata viongozi wa upinzani.
“Baada ya uchaguzi mkuu wa 2020 tulikutana na viongozi wenzangu wa upinzani, akiwemo Zitto (Kabwe-Kiongozi wa ACT-Wazalendo) Lissu (Tundu-mgombea urais), Godbless Lema, Boniface Jacob na Maalim Seif (Sharif Hamad-mgombea urais Zanzibar alituma mwakilishi).
“Tulishauriana kwa uchaguzi ule yote tulioyapitia? Tusikubaliane na matokeo ya mchakato ule. Tulikubaliana tuwaombe Watanzania tufanye maandamaano ya amani, kupinga uchaguzi wa mwaka 2020,”amesema Mbowe.
Mbowe ambaye ni mwenyekiti mwenza wa DUA, amesema baada ya kikao hicho, alikamatwa na kupelekwa kusikojulikana.
“Nilifungwa kitambaa cheusi usoni na kupelekwa nisikokujua na baada ya siku tatu niligundua nipo Bagamoyo (Pwani), wenzangu kina Lema, Jacob sikujua wapo wapi baada ya kukamatwa, kila mmoja alipelekwa kivyake, lakini mimi nikajikuta nipo Bagamoyo,” amesema Mbowe.
Hata hivyo, Mbowe amesema Lissu hakukamatwa baada ya kukimbilia ubalozi wa Ujerumani kutafuta hifadhi ya ukimbizi na alifanikiwa, kisha kuondoka nchini.
Lissu ambaye ni makamu mwenyekiti wa Chadema, bara aliomba hifadhi katika ubalozi wa Ujerumani tangu Novemba 2, 2020 akidai kutishiwa maisha yake, lakini Novemba 10, 2020 aliondoka kwenda Ubeligiji alikokuwa akiishi tangu Januari 2018 na mpaka sasa yupo huko.
Mbowe amesema baada ya muda mfupi, Lema aliachiwa kwa dhamana na kuondoka kwenda Canada ambako anaishi hivi sasa na familia yake.
“Mimi nilijaribu kukomaa kidogo, lakini niliondoka kwenda Kenya kisha nikapata kibali cha kuishi Dubai,” amesema Mbowe.
Novemba Mosi Jeshi la Polisi lilitangaza kumkamata Mbowe na wenzake kwa madai kuwa walikuwa katika kikao huku wakiwatuhumu kupanga mipango ya kufanya maandamano yasiyo na kikomo kuanzia Novemba 2, 2020.
Maandamano hayo yalitangazwa na Mbowe, Zitto na Lissu lengo likiwa kushinikiza uchaguzi mkuu wa Oktoba 28, 2020 urudiwe kwa kuwa haukuwa huru na wa haki.