Buchosa. Mhitimu wa darasa la saba katika shule ya msingi Kanyala Wilayani Sengerema Mkoa wa Mwanza, Roda Majaliwa (14) amepoteza maisha kwa kuliwa na mamba wakati anaoga katika ziwa Victoria.
Tukio hilo ni la pili kutokea ndani ya miezi mitatu mwaka huu, ambapo Oktoba 28 mwaka huu Mashauri Minani (17) aliyekuwa anasoma kidato cha kwanza shule ya sekondari Maisome alipoteza maisha kwa kuliwa na mamba wakati anaoga katika ziwa hilo.
Akizungumza na Mwananchi leo Desemba 5, Mwenyekiti wa Kijiji cha Kanyala, Gacha Paul amesema tukio hili limetokea Desemba 4 mwaka huu majira ya saa 5 asubuhi wakati marehemu alipokuwa akioga ziwani.
“Baada ya tukio hilo jamii ya Kijiji cha Kanyala walianza msako wa kusaka mamba na kufanikiwa kuupata mwili wa mhitimu huyo ukiwa umejeruhiwa vibaya.
“Mazishi yake yanafanyika leo Desemba 5 kijijini hapa,” amesema Paul.
Jacob Ernest ambaye ni mkazi wa kijiji cha Kanyala, ameiomba Serikali kutoa elimu kwa wakazi wanaoishi kazi ya ziwa hilo ili kuepusha madhara zaidi.
"Maisha ya watu yanakatizwa na mnyama mamba hivyo serikali inatakiwa kuona namuna ya kuisadia jamii ili kuepuka vifo vya watu ambao ni nguvu kazi ya Taifa,” amesema Ernest.
Hivi karibuni, Mkuu wa Wilaya ya Sengerema, Senyi Ngaga katika ziara zake za kuhasisha masuala ya maendeleo aliwaasa wananchi kuacha kuoga ziwani ili kuepuka kuliwa na mamba ambao wamekuwa katika mawindo ya kutafuta chakula.
"Tunapaswa kuchukuwa tafadhari tunapofanya shughuli ndani ya ziwa Victoria ili kuepuka madhara ya kuliwa na mamba,” amesema Ngaga.