MLINZI wa eneo la kuhifadhia mitungi ya gesi eneo la Tegeta Scanska, Kinondoni, Dar es Salaam, Salim Haji, anadaiwa kuuawa kwa kupigwa risasi na mmiliki wa biashara hiyo, kisha mwili wake kuchukuliwa na kupelekwa kusikojulikana usiku.
Kamanda wa Polisi Kanda maalum ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro.
Mlinzi huyo ambaye ni mwajiriwa wa kampuni ya ulinzi ya Homasa, anadaiwa kuuawa Novemba 20, mwaka huu, akiwa kazini kwa mmoja wa wateja wa kampuni hiyo na mpaka sasa ndugu zake wanatafuta mwili wake na hawajauona.
Kwa mujibu wa mlinzi mwenzake aliyejitaja kwa jina moja la Julius, mwenzake aliuawa akiwa lindoni ndani ya eneo la kazi, kati ya saa 4:00 na saa 5:00 usiku wakati yeye akiimarisha ulinzi getini na mwenzake (anayedaiwa kuuawa) akiimarisha ulinzi kwa ndani.
“Ilikuwa saa tano kama kasoro dakika 10 au 12, waliingia wafanyakazi wa kusambaza mitungi ya gesi wakiwa na usafiri wa pikipiki na baada ya dakika tano, nikasikia geti linavutwa, alikuwa bosi wa hilo eneo la gesi tunapolinda. Alipoingia ndani akaninyooshea bastola akasema anawafuata wale waliorudisha mitungi ya gesi huku akininyooshea bastola,” alisema Julius
“Alipowafuata, dakika chache nikasikia milio ya risasi, nikawaona wale wafanyakazi wake waliokuwa wamerudisha gesi wakawa wanakuja wanakimbia. Nilipowauliza, wakaniambia bosi wao anarusha risasi na nilipowauliza sababu ya kufanya hivyo, wakaendelea kukimbia huku wanatoka.
“Mara nikaona anakuja hadi niliko getini, akaniambia niweke silaha chini niondoke la sivyo atanipasua, nikamwambia siondoki, nalinda mali hapa. Akaendelea kunisisitiza nikagoma. Nilipoona hivyo nikageuka kwa nyuma kwa nje hapo hapo getini, akaninyooshea bastola, kidogo akapiga risasi juu. Wakati huo nikaona mke wake anaingia na gari ndani huku akimsisitiza asipige risasi.
“Baada ya kuona anaendelea kupiga risasi juu, mimi nikatoka nikaanza kukimbia ili nikawapigie simu viongozi wangu ambao baada ya dakika 20 wakawa wamefika eneo la tukio. Wakati huo wa purukushani zote hizo zikiendelea, sikumwona askari mwenzangu kutokeza japokuwa yeye ndiye alikuwa kwa ndani zaidi maana ni eneo kubwa.
“Baada ya kiongozi wangu kufika, nilimwambia atangulie, nikabaki nyuma na alipofika yeye akaona gari imepakiza mtu na imetoka. Baada ya wao kuondoka tukazunguka mle ndani kuanza kumwita mlinzi mwenzangu, hatukumuona. Tulipiga simu yake mwanzoni ilikuwa inapokelewa halafu hakuna anayeongea, kwa hiyo tulichoambulia kuona ni damu zikiwa zimetapakaa chini,” alisimulia.
Alisema, majira ya saa 6:00 usiku huo huo, alirudi tena mke wa mmiliki wa gesi akiwa anatembea kwa miguu na walipomuuliza nini kinaendelea kwa mume wake, aliwajibu kiufupi kwamba ni mambo ya dunia.
“Dakika chache, mume wake naye akarudi tena akitembea kwa miguu, ananiambia kwamba nifukie ile damu iliyokuwa imetapakaa pale chini, nikamwambia sifukii mpaka polisi waje wafanye uchunguzi tujue ni ya nini.”
Alisema baada ya kumtafuta mwenzake bila mafanikio, walikwenda kituo cha polisi Madale kutoa taarifa na wakapatiwa namba MBD/CID/PE/34/2022.
“Cha kushangaza tulipofika polisi ilikuwa saa 9:30 usiku, tulipoanza kuandikisha maelezo yetu tukamwona yule bosi aliyefanya tukio la kupiga risasi naye amekuja. Tukaenda tena eneo la tukio na polisi wakachukua taarifa na wakafungua jalada letu,” alisema.
Alisema tangu kutokea kwa tukio hilo, wamekuwa wakifuatilia polisi kujua upelelezi ulipofikia lakini wanaambiwa bado upelelezi unaendelea.
“Kibaya zaidi wanatuambia hivyo wakati hata hatujui mwenzetu yuko wapi na wakati mwingine tunarushiwa maneno makali na baadhi ya askari jambo ambalo linatutia mashaka. Ndugu nao wanataka mtoto wao,” alisema Julius.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Ulinzi ya Homasa, Imani Mileka, alisema alipata taarifa ya kutokea tukio hilo usiku wa Novemba 20 kuamkia Novemba 21 kwamba mteja wake wa mitungi ya gesi (anamtaja jina lake), amefyatua risasi, eneo la tukio kumetapakaa damu na mlinzi mwenzao hayupo.
“Nilipofika pale nilikuta damu na sikujua ni ya nani kwa wakati ule. Kwa kawaida lindo hilo huwa lina walinzi wawili, mmoja anashika silaha na mwingine rungu, kwa hiyo mlinzi Salimu ambaye haonekani mpaka leo yeye ndiye alikuwa anashika rungu kwa ndani ambaye sikumuona nilipofika na mwenzake aliyepona akiwa getini.
“Nilipomuuliza sababu ya kufyatua risasi, alisema eti alipomfukuza mlinzi getini, walikwenda vibaka wakataka kumkata mapanga, kwa hiyo akavunja mguu wa mmoja wapo lakini wakapakizana kwenye boda boda wakakimbia. Na hata tulipomuuliza alipo mlinzi wetu mmoja akawa mkali na kuniambia nimwache,” alisema.
Alisema baada ya tukio hilo, mteja wake alivunja mkataba wa kampuni yake kuendelea kufanya kazi nao.
Mjomba wa Mlinzi anayedaiwa kuuawa, Bakari Mdoe, alisema tangu kijana wao alipokwenda kazini Novemba 20 hawakumwona tena.
Nipashe ilimpigia simu Kamanda wa Polisi Kanda maalum ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro ili kujua endapo ana taarifa ya tukio hilo lakini simu zake hazikupokewa