Msanii Diamond Platnumz.
UAMKIE muziki, uheshimu muziki siyo mwepesi kama unavyofikiria unaweza kuishi nao milele, Ijumaa linakupa kiyo ichukue ikusaidie.
Msanii Diamond Platnumz amenyoosha mikono kwa kusema:“Sina ndoto za kuimba milele, nataka kuwa Mfanyabiashara mkubwa bilionea.”
Baadhi ya watu wameipokea kauli yake kwa mshtuko na maneno haya: “Anajuwa kwenye mziki hana jipya wamemshauri vizuri,” mchangiaji wa mitandaoni Muksini Mbaruku anaandika katika komenti yake.
Kwenye moja ya mahojano yake mwishoni mwa wiki iliyopita jijini Dar es Salaam, Diamond aliwagawa watu kuhusu kauli yake hiyo na kuzua gumzo zito mitandaoni.
Wapo waliosema kuwa hana jipya kimuziki ndiyo maana ameanza ‘kutangaza amani’ mapema ili kukwepa aibu pale muziki wake utakapokosa soko mazimaaa.
“Kashapotea anajitetea huyo,” mtoa maoni mwingine kwenye mtandao ya YouTube aliandika komenti.
Katika siku za hivi karibuni kumekuwepo na vita ya kimuziki kati ya msanii huyo na ”zao lake kisanaa” Harmonize kuwa mwanafunzi wake huyo amekuwa juu kimuziki kuliko mwalimu ambaye ni Diamond.
Kama inavyofahamika kabla ya Harmonize kuanzisha Lebo yake ya Konde Gang, alipita kwenye Lebo ya Wasafi Classic Baby (WCB) ya bosi Diamond na kulelewa hapo kwa miaka kadhaa.
Hata hivyo, tangu ajitenge WCB baadhi ya watu akiwemo Harmonize mwenyewe wamekuwa wakijinasibu kuwa juu kimuziki kuliko Diamond kutokana na kuendesha harakati za kisanaa zisizokuwa na wapambe.
Alipofyatua albam yake ya ‘Made For Us’ na kuweza kufikisha watazamaji milioni 30 kwenye mtandao wa BoomPlay kwa muda mfupi, Harmonize alionesha furaha yake kwa kusema mafanikio yake hayako nyuma ya ‘chawa’ wala nguvu ya vyombo vya habari, akimtaja kimafumbo Diamond mwenye vyombo vya habari na ‘chawa’ kibao.
Mshtuko na gumzo la Diamond kuacha muziki limekoleza mitazamo tofauti kwa wadau wa muziki kwani wapo wanaofikiri huenda msanii huyo anakimbia ushindani ambao unaletwa kwake hivi sasa na wasanii wachanga wanaoonekana kufanya vizuri kisanii huku wengine wakimsapoti kwa fikra hizo za kimaendeleo.
Sifael Paul mwandishi wa habari za burudani kwa miaka mingi alisema alipoongea na Ijumaa kuhusu kauli ya Mondi:
“Nimeshuhudia wasanii wengi waliokuwa moto wakiporomoka kimuziki na kugeuka kuwa wabwia unga.
“Hii ina maana gani? Kama mwanamuziki hatauacha muziki akifikia kikomo chake, muziki wenyewe utamwacha na aibu tele.
“Msanii anayefikiria kuacha muziki kama Diamond, mara nyingi hubaki salama kimaisha kwani anakuwa amejiandaa, kama kuacha muziki na kufanya biashara au kazi nyingine ya kumuingizia kipato.
“Wasanii ambao huachishwa kazi na muziki wenyewe kwa umri na shoo zao kubuma hujikuta kwenye nyakati ngumu za kimaisha kiasi cha kuonekana kama wendawazimu.
“Si busara kuwataja kwa majina walioachwa na muziki, chunguza mwewewe wasanii waliokuwa moto sio Bongo hata nje ya nchi leo wakoje kimaisha, ni kama wamedata.”
Kauli ya Diamond kuachana na muziki na kugeukia biashara amekuwa akiitoa mara kwa mara ambapo mwaka 2018 pia aliwahi kusema kauli kama hiyo alipokuwa akizindua moja ya kipindi kwenye radio moja hapa nchini.
Tuma maoni yako kuhusu uamuzi huu wa Diamond kuuweka kando muziki muda ukifika na kugeukia biashara kwa kutembelea mtandao wa Instagram wa globaltvonline.