Wakati maumivu ya kuondokewa na Piarisi Hiza, aliyekuwa mama wa watoto wawili yakiwa hayajasahaulika ndani ya familia, taarifa zinadai mume wa marehemu John Mnyilaha aliyekuwa mshukiwa wa kwanza wa kifo chake ameachiwa huru.
Dar es Salaam. Wakati maumivu ya kuondokewa na Piarisi Hiza, aliyekuwa mama wa watoto wawili yakiwa hayajasahaulika ndani ya familia, taarifa zinadai mume wa marehemu John Mnyilaha aliyekuwa mshukiwa wa kwanza wa kifo chake ameachiwa huru.
Taarifa kutoka ndani ya familia ya Piarisi zinadai mwanaume huyo baada ya kuachiwa inasemekana yuko nchini Afrika Kusini.
Hilo linatokea ikiwa zimedpita siku 62 tangu Piarisi afariki dunia Oktoba 2, mwaka huu ndani ya chumba alichokuwa amelala na mumewe, Tabata Segerea jijini Dar es Salaam kwa kile kilichoelezwa alijinyonga.
Alipoulizwa juu ya suala hilo, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro alisema, “ngoja nifuatilie suala hili nilielewe ili nipate cha kujibu.”
Awali, Mwananchi lilizungumza na ndugu wa Piarisi aliyedai taarifa za mume wa marehemu kuwa huru zilithibitishwa na ndugu zake katika kikao cha familia baada ya kubanwa.
Alisema ndugu hao walifika katika kikao kuomba kushiriki katika misa ya kumuombea Piarisi iliyopangwa kufanyika Desemba mwaka huu Lushoto mkoani Tanga ambako mwili ndugu yao ulizikwa.
Alisema walipofika kikaoni waliulizwa ndugu yao yuko wapi baada ya kuelezwa walikwenda kumuangalia katika kituo cha polisi Stakishari alichokuwa akishikiliwa awali hawakumkuta ndipo walipoambiwa alihamishiwa gereza la Segerea.
Alieleza ndugu wa mwanamke waliwapatia masharti ya wao kushiriki misa hiyo kuwa ni lazima familia ianzie gereza la Segerea kumuona mtuhumiwa kabla ya kwenda Lushoto katika misa.
Awali, baada ya taarifa za mwanaume huyo kuachiwa huru na watu kukiri kumuona mtaani zikisambaa walikwenda kituo cha Stakishari alichokuwa akishikiliwa awali, lakini hawakumkuta huku wakidai waliona ametoka kusaini kituoni hapo ikiwa na maana kuwa yuko nje.
Pia kabla ya kumtoa polisi inasemekana ulipitishwa mchango wa fedha, ili kufanikisha shughuli hiyo na baadhi ya taarifa zilizokuwa zinawafikia zilikuwa zikitoka upande wa mwanaume.
“Kuna wengine ndani ya familia yao wao wenyewe hawapendi kile inachoendelea, hivyo wamekuwa wakituambia kwa sababu wao wako kinyume na kile kinachofanyika.
“Tuliwaambia hata watoto wale wawili ni wa kwao, wakitaka kutujua watatutafuta wao wenyewe,” alisema.
Marehemu aliacha watoto wawili, wa kiume akiwa na miaka miwili na mdogo ambaye ni wa kike alikuwa na miezi tisa wakati mama yake akifariki.
Haya yote yanatokea ikiwa tangu tukio hilo la mauaji yaliyogubikwa na utata, upande wa marehemu unadai haukuwahi kuitwa mahakamani wala kupewa taarifa yoyote juu ya mwenendo wa upelelezi.
Wawili hao mume na mke wanadaiwa kutoka kwenda kujirusha siku ya Jumamosi ya Oktoba 1 mwaka huu na walirudi nyumbani asubuhi ya Oktoba 2 na waliingia chumbani moja kwa moja kulala.
Ilipofika saa tano asubuhi, John ambaye ni mume wa marehemu alimgongea mlango dada wa kazi aliyefahamika kwa jina moja la Aneth na kumuambia dada yake amejinyonga chumbani, jambo ambalo liliacha maswali mengi.