Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres ametangaza uteuzi wa Elizabeth Maruma Mrema kutoka nchini Tanzania kuwa Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Mazingira (UNEP).
Taarifa iliyotolewa Jana Desemba 27,2022 na msemaji wa katibu mkuu wa Umoja wa mataifa mjini New York Marekani, Guterres amesema Mrema atamrithi Joyce Msuya ambaye pia ni Mtanzania aliyeteuliwa hivi karibuni kuwa Katibu Mkuu Msaidizi wa Masuala ya Kibinadamu na Naibu Mratibu wa Misaada ya Dharura katika ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu Masuala ya Kibinadamu (OCHA).
Elizabeth Mrema amewahi kuhudumu kama Katibu Mtendaji wa Sekretarieti ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Bayoanuai (CBD), yenye makao yake mjini Montreal, Canada.
Aidha, amewahi kuwa Kaimu Katibu Mtendaji wa Sekretarieti ya CBD na Mkurugenzi wa Kitengo cha Sheria katika shirika la UNEP huko Nairobi, Kenya, pamoja na kuwa Katibu Mtendaji wa Sekretarieti ya Mkataba wa Sekretarieti ya Wanyama Wanaohama yenye makao yake makuu mjini Bonn, Ujerumani.
Elizabeth Mrema amewahi pia kufanya kazi katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ya Tanzania kabla ya kushika nyadhifa nyingine kimataifa.