Janusz Walus, mshambuliaji wa siasa kali za mrengo wa kulia aliyemuua shujaa wa kupinga ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini Chris Hani amedungwa kisu gerezani, maafisa wanasema.
Kudungwa kisu kwa Janusz Walus kunakuja siku chache kabla ya kuachiliwa kwa msamaha baada ya takriban miaka 30 jela.
Inadaiwa alidungwa kisu na mfungwa mwingine na hali yake inaendelea vizuri.
Walus, 69, alimpiga risasi Bw Hani mwaka wa 1993 katika jaribio lililofeli la kuvuruga mpito wa Afrika Kusini kutoka utawala wa wazungu wachache hadi utawala wa kidemokrasia.
Mauaji hayo bado yanaibua hisia kali nchini Afrika Kusini. Bw Hani alichukuliwa kuwa mwanasiasa maarufu zaidi baada ya mwanasiasa aliyepinga ubaguzi wa rangi Nelson Mandela.
Serikali ya Afrika Kusini na mjane wa Bw Hani Limpho walipinga vikali majaribio ya Walus kupata uhuru wake. Lakini katika uamuzi wa tarehe 21 Novemba, mahakama ya juu zaidi ya Afrika Kusini iliamuru kuachiliwa kwake ndani ya siku 10, ikisema kukataa kwa waziri wa sheria kumpa msamaha "hakuna mantiki".
Katika taarifa fupi, idara ya magereza ilisema inaweza kuthibitisha "tukio la bahati mbaya la kuchomwa kisu" linalomhusisha Walus. Maafisa wa afya walikuwa wakimpa "huduma muhimu", iliongeza.
BBC ina taarifa kuwa mshambuliaji wake alijaribu kumdunga kisu kwenye moyo.
Shambulio hilo lilijiri baada ya mnara wa kumbukumbu ya Bw Hani kuharibiwa siku ya Jumamosi katika makaburi aliyozikwa. Chama tawala cha African National Congress (ANC) na washirika wake walielezea tukio hilo kuwa ni "shambulio la uchochezi", na "sawa na muendelezo wa mauaji ya Chris Hani kaburini".
Walus alimuua Bw Hani alipokuwa akiokota magazeti nje ya nyumba yake mnamo Aprili 1993 kwa kumpiga risasi kwa kumlenga moja kwa moja.
Walus alikamatwa na kuhukumiwa kifo. Hukumu hiyo ilibadilishwa kuwa maisha baada ya Afrika Kusini kufuta hukumu ya kifo.
Mpiganaji huyo wa kupinga ubaguzi wa rangi mwenye umri wa miaka 50 alikuwa kiongozi wa SACP na mwanachama mkuu wa tawi la kijeshi la ANC.
Walus ni mhamiaji kutoka Poland ambaye uraia wake wa Afrika Kusini ulibatilishwa mwaka wa 2017. Baadhi ya raia wa Afrika Kusini wametaka afurushwe ili kuzuia machafuko ya wenyewe kwa wenyewe.
Hata hivyo, serikali imefutilia mbali hilo, ikisema atatumikia msamaha wake nchini Afrika Kusini.
Utawala wa wazungu wachache nchini Afrika Kusini ulimalizika mwaka 1994, na Bw Mandela kuwa rais wa kwanza mweusi wa nchi hiyo